MALI-CANADA

Canada kutuma wanajeshi na ndege za kivita Mali

Picha ikiwaonesha wanajeshi wa Ufaransa wanaoshiriki operesheni Barkhane nchini Mali, hapa wakiwa kwenye mji wa Timbamogoye
Picha ikiwaonesha wanajeshi wa Ufaransa wanaoshiriki operesheni Barkhane nchini Mali, hapa wakiwa kwenye mji wa Timbamogoye Pascal Guyot, AFP

Nchi ya Canada imesema itatuma ndege kadhaa za kivita na zile za kusafirisha mizigo pamoja na wanajeshi watakaotoa mafunzo nchini Mali katika kipindi cha miezi 12 kusaidia operesheni inayoendelea kufanywa na walinda amani wa umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa ulinzi wa Canada, Harjit Sajjan amewaambia waandishi wa habari kuwa kikosi hicho maalumu kitajumuisha Helkopta mbili kubwa za kivita ambazo zinahitajika kwa sasa kwaajili ya usafirishaji pamoja na helkopta nyingine nne za kuendesha mashambulizi na kulinda misafara ya walinda amani.

Hata hivyo tarehe rasmi ya operesheni hii ya kwanza ya Canada barani Afrika tangu misheni yake ya nchini Rwanda na Somalia katika miaka ya 1990 pamoja na idadi kamili ya wanajeshi watakaotumwa, haijawekwa wazi.

Hakikisho hili la Canada limekuja baada ya mwaka uliopita Serikali ya Ottawa kusema kuwa ingetuma ndege za kivita na zile za usafirishaji kusaidia operesheni za ukanda mjini Entebbe Uganda pamoja na kuweka tayari kikosi chake kitakachosaidia operesheni za umoja wa Mataifa kilichokuwa na wanajeshi 200.

Waziri wa mambo ya nje wa Canada Chrystia Freeland amesema kuwa kikosi kitakachotumwa nchini Mali kitajumuisha wanawake ili kufikia lengo la usawa wa kijinsia kwenye operesheni za umoja wa Mataifa za kulinda amani.

"Moja ya vipaumbele vyetu ni kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika operesheni za kulinda amani,: alisema waziri Freeland.

Hivi sasa wanawake wanaunda asilimia 3.7 ya wanajeshi wa kulinda amani na asilimia 9.5 ya polisi wanaolinda amani.

Umoja wa Mataifa hivi sasa unalenga kuongeza maradufu idadu ya wanawake wanaoshiriki operesheni za kulinda amani ifikapo mwaka 2020.

Operesheni za nchini Mali ni moja ya operesheni hatari za umoja wa Mataifa, ambapo jumla ya walinda amani 150 wameuawa tangu mwaka 2013.

Wakati mmoja nchi ya Mali ilisifika kwa kuwa taifa lililostawi demokrasia na utawala bora, limeshuhudia mapinduzi ya kijeshi, vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kuongeza kwa makundi ya kijihadi.

Wanadipolomasia wawili wa Canada walitekwa na kushikiliwa mateka kaskazini mwa Mali mwaka 2009.

Makundi ya kijihadi ya kiislamu yenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda walichukua maeneo ya kaskazini mwa Mali kwenye mwaka 2012 lakini walifurushwa kwa kiwango kikubwa na majeshi ya Ufaransa Januari mwaka 2013.

Mwezi Juni mwaka 2015, Serikali ya Mali ilitiliana saini makubaliano ya mkataba wa amani na baadhi ya makundi yenye silaha, lakini makundi mengine ya kijhadi bado yanafanya shughuli zao kaskazini mwa nchi hiyo.

Miezi ya hivi karibuni wanajihadi wamezidisha shughuliz zao katikati mwa nchi ya mali wakilenga vikosi vya Serikali na vile vya kigeni.

Jumla ya walinda amani wa nne wa umoja wa mataifa waliuawa na wengine wa nne walijeruhiwa mwezi Februari mwaka huu wakati gari walilokuwa wakitumia kukanyaga bomu la kutegwa ardhini.