DRC-UN-EU

EU yasikitishwa na kauli ya Serikali ya Kinshasa kuhusu mkutano wa Geneva

Jengo la UNICEF lililoko mjini Geneva.
Jengo la UNICEF lililoko mjini Geneva. REUTERS/Denis Balibouse

Umoja wa Ulaya umesema unaguswa na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya nchi hiyo kutangaza kuwa itakataa kupokea kiasi cha dola za Marekani bilioni 1 na laki 7 ambazo ni msaada wa kimataifa.

Matangazo ya kibiashara

Mvutano wa maneno umeibuka kati ya umoja wa Mataifa na Serikali ya DRC baada ya utawala wa Kinshasa Ijumaa ya wiki iliyopita kusema haitashiriki mkutano wa kimataifa wa kuisaidia nchi hiyo fedha za misaada ya kibinadamu mjini Geneva, Uswis, Serikali ikisema tatizo la kibinadamu limeongezwa chumvi kuliko hali halisi.

“Umoja wa Ulaya unaguswa na kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini DRC,” amesema mkuu wa masuala ya kibinadamu kutoka umoja wa Ulaya Christos Stylianides wakati akizungumza na wanahabari kwenye mji wa Goma.

“Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kila uchao na kwa bahati mbaya nimeona madhila makubwa na uhitaji wa haraka wa misaada na hali nchini DRC sio kama ilivyozoeleka.”

Waziri mkuu wa DRC Jose Makila alinukuliwa siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita akisema umoja wa Mataifa umoengeza chumvi na kwamba mashirika yake ya misaada na asasi za kiraia zimekuwa zikifanya propaganda ya kuichafua nchi yake.

“Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapinga na haitashiriki kwenye mkutano wa Geneva” tarehe 13 April, alisema waziri mkuu Makila.

Umoja wa Mataifa umetangaza janga la kibinadamu nchini DRC kufikia ngazi ya 3, hii ikiwa ni ngazi ya juu ya uhitaji wa misaada ya dharula.

Stylianides anatarajiwa kukutana na maofisa wa Serikali akiwemo waziri wa mambo ya nje wa DRC ambapo amesema atajaribu kumshawishi kuhusu umuihimu wa nchi hiyo kushiriki mkutano wa Geneva.

Watu wanaokadiriwa kufikia milioni 13 na laki 1 nchini DRC wanahitaji msaada wa kibinadamu wakiwemo watu milioni 7 na laki 7 ambao wanakabilia na njaa, imesema taarifa ya baraza la usalama la umoja wa Mataifa.

Shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na watoto nalo mwaka uliopita lilionesha kuguswa na kudai kuwa watoto zaidi ya laki 4 wako hatarini kufa kwenye mkoa wa kati wa Kasai ambao unashuhudia vurugu.

Watu zaidi ya elfu 3 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya milioni 1 na laki 4 wamepoteza makazi yao.