DRC-UN

Machafuko ya Kasai mtihani mwingine kwa Serikali ya DRC

Machafuko kwenye mkoa wa Kasai yamesababisha vifo vya watu 3,300 na wengine milioni 1 kukimbia nchi yao.
Machafuko kwenye mkoa wa Kasai yamesababisha vifo vya watu 3,300 na wengine milioni 1 kukimbia nchi yao. AFP/File

Moja ya mambo yanayoumiza kichwa na kuikabili tume ya umoja wa mataifa nchini DRC, MONUSCO wakati huu inapotarajiwa kuongezewa muda ni suala la vurugu za kikabila na kuzorota kwa hali ya kibinadamu kwenye mkoa wa Kasai.

Matangazo ya kibiashara

Eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini limetumbukia kwenye machafuko tangu mwezi septemba mwaka 2016 baada ya wanajeshi kumuua kiongozi wa kijadi wa eneo hilo Kamwina Nsapu.

Mapigano yamesababisha vifo vya watu 3000 na wengine zaidi ya milioni 1 na laki 4 kukosa mahali pakuishi, hii ni kwa mujibu wa takwimu za kanisa Katoliki nchini DRC.

Njaa pia imeukumba mkoa huo kutokana na mavuno duni au mazao yao kuharibiwa kutokana na mapigano.

Kwa mujibu wa shirika la umoja wa mataifa linalohusika na watoto UNICEF linasema watoto zaidi ya laki 4 wanakabiliwa na utapia mlo na wako hatarini kufa.

Ripoti za mauaji, kukamatwa kwa watu na vitendo vya utekaji ambapo pesa nyingi hudaiwa ni mambo ambayo yako wazi kwenye mkoa huo, huku lawama zikielekezwa kwa Serikali na wapiganaji wa Nsapu kutokana na ukabila.

Wataalamu wa magharibi wanasema kuwa "karibu makundi 14 ya waasi yanafanya kazi kwenye eneo hilo,"

Gavana wa mkoa wa Kasai Marc Manyanga ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa makundi mengi yanatoka kwenye vijiji na jamii ya Kamwina Nsapu kutoka kabila la Luba.

Vurugu za Kikabila:

Mwalimu mmoja Maxime Salaka anasema baada ya vikosi vya Serikali kuingia kwenye mji huo "mgogoro haukuisha lakini ukachukua uelekeo mpya wa kikabila."

Kundi moja linaunda kundi la Bana Mura kutoka kabila la Tshokwe na kundi jingine la Ecurie Mbembe lililoundwa na jamii ya watu wa kabila la Pende.

Mzozo wa Kisiasa:

Hata hivyo wachambuzi wanasema Serikali dhaifu iliyozungukwa na sintofahamu ya mustakabli wa siasa za nchi hiyo ni miongoni mwa matatizo yanayoikabilia DRC.

Uchaguzi wa urais umeahirishwa kwa zaidi ya mara mbili tangu rais Joseph Kabila alipotakiwa kuondoka madarakani mwaka 2016.

Tarehe mpya ya uchaguzi imepangwa kuwa ni tarehe 23 Desemba ya mwaka huu, lakini tayari kumezuka hofu ikiwa uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa na ikiwa rais Kabila ataondoka madarakani au la.

Katika sintofahamu zote hizi tume ya MONUSCO ambayo inawanajeshi zaidi ya elfu 18 na 300 ambao wanajumuisha Polisi na raia nchini DRC kunaifanya kuwa tume yenye kikosi kikubwa cha kulinda amani duniani na sasa kinakabiliwa na chan gamoto ya kudhibiti usalama nchini DRC.