DRC-USALAMA

Wakimbizi wa ndani wa Ituri waanza kurudi nyumbani

Watoto waliokimbia kufuatia machafuko ya Ituri wakiwa katika kambi huko Bunia, Aprili 9, 2018.
Watoto waliokimbia kufuatia machafuko ya Ituri wakiwa katika kambi huko Bunia, Aprili 9, 2018. REUTERS/Goran Tomasevic

Hali ya utulivu imeanza kurejea katika mkoa wa Orientale, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mkuu wa mkoa huo Abdhallah Pene Mbaka ameanza kuhimiza wakimbizi wa ndani kurejea nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya watu 340 000, kwa mujibu wa shirika la kihisani la Umoja wa Mataifa OCHA, walilazimika kuyahama makazi yao baada ya mfululizo wa mauaji na vurugu kati ya watu kutoka jamii ya Hema na Lendu.

Machafuko hayo yalisababisha watu 250 kupoteza maisha tangua mwezi Desemba mwaka 2018, kwa mujibu wa OCHA. Lakini mashirika ya kiraia nchini DRC yamesem azaidi ya watu 250 waliuawa katika machafuko hayo. Kwa wiki tatu, vurugu hizo zimepungua kwa kasi, baada ya kutumwa kwa askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo (Monusco) kwa ushirikiano na jeshi la DRC. Tangu siku ya Jumamosi ya wiki iliyopita viongozi wa mkoa walianza zoezi la kutambua wakimbizi wanaotaka kurejea nyumbani kwa hiari yao.

Katika siku tatu, viongozi wa mkoa wameorodhesha wakimbizi 4,700ambao wanataka kurudi nyumbani na operesheni inaendelea. Wakati huo huo, wawakilishi wawakimbizi hao, katika siku za hivi karibuni, watatembelea maeneo yaliyoathiriwa ili kutathmini hali ya usalama.

"Hali ya utulivu imeanza kurejea, lakini siwezi kusema kuwa hali imekua shwari moja kwa moja, "amesema Mkuu wa mkoa Abdhallah Pene Mbaka.

"Uharibifu ni mkubwa sana, vijiji vyote vilichomwa moto. Basi nini cha kufanya kwa watu ambao wamepoteza nyumba zao? "Kuna msaada ambao wao watapewa kutoka kwa serikali ya mkoa (lakini pia) Serikali kuu, " ameongeza Abdhallah Pene Mbaka.

Zaidi ya watu 43,000 walikimbilia nchini Uganda. Siku ya Jumanne wiki hii, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Leïla Zerrougui alikuwa Bunia kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye nafasi hiyo. Baada ya mkutano na mkuu wa mkoa, alisisitiza juu ya haja ya kujua sababu za msingi za mgogoro huu na kufanya kazi kwa lengo la kuboresha maridhiano kati ya jamii hizi mbili.