Jeshi la Nigeria lashtumiwa kuwabaka wanawake na watoto

Amnesty International yainyooshea kidole cha lawama jeshi la Nigeria kwa kuwabaka wanawake na watoto.
Amnesty International yainyooshea kidole cha lawama jeshi la Nigeria kwa kuwabaka wanawake na watoto. AFP

Shirika la kimataifa linalotetea Haki za Binadamu, Amnesty International, linalishtumu jeshi la Nigeria kuwa limekuwa likiwabaka wanawake na watoto katika harakati zake za kuwasaka wanamgambo wa kundi la Boko Haramu Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti yake mpya Amnesty International inasema kuwa jeshi la serikali katika jimbo la Borno limehusika na vitendo vya ubakaji na kulazimisha suala la mahusiano na wanawake waliokimbia machafuko katika kambi za wakimbizi.

Hata hivyo ripoti imeendelea kueleza kuwa wanawake wanadhaniwa walikuwa wake wa wapiganaji wa Boko Haram watano kati yao wamefariki,huku watoto 32 wakidaiwa kufa pia.

Amnesty wanawatuhumu baadhi ya wanajeshi kufanya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake katika kambi za wakimbizi wa ndani kama malipo kwa msaada wanaotoa.

Amnesty International inasema imefanya uchungui na kuweza kuhoji watu 250 kati ya mwaka 2016 na 2018.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kuwa baadhi ya wanajeshi nchini Nigeria wanajinufaisha kimapenzi kwa kutumia mazingira magumu ya chakula yanayowawakabili wakimbizi hao.

Msemaji wa jeshi la Nigeria amefutilia mbali ripoti hiyo na kusema kuwa madai hayo hayana msingi wowote na ni uzushi unaolenga kupata matope jeshi la Nigeria.