CAR-MINUSCA-USALAMA

Askari wa Tanzania auawa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Msafara wa magari ya kijeshi ya Minusca kwenye barabara ya Bambari kuelekea Ippy.
Msafara wa magari ya kijeshi ya Minusca kwenye barabara ya Bambari kuelekea Ippy. © RFI/Pierre Pinto

Askari mmoja wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania ameuawa na wengine saba walijeruhiwa wakati msafara wao uliposhambuliwa kwa risasi na watu wenye silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, viongozi wa Umoja wa Mataifa wamesema.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema washambuliaji ambao ni wa wanamgambo wa Siriri, walishambulia msafara wa askari wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumapili katika kijiji cha Dilapoko, kaskazini magharibi mwa Mambéré. -Kadeï.

Mmoja wa waliojeruhiwa yuko katika hali mbaya katika hospitali ya mjini Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo, ambapo walinda amani wengine watatu walijeruhiwa pia na wanapewa matibabu katika mji wa Berberati, Bw Dujarric ameongeza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mashambulizi hayo, ambayo yamekamilisha idadi ya Walinda amani wanne ambao wameuawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka huu.

Minusca, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, una askari na polisi 12,000 waliotumwa katika nchi hiyo inayoendelea kukumbwa na migogoro tangu mwaka 2013.