DRC-UCHAGUZI-SIASA

DRC: Raia waishio ugenini hawatopiga kura

Zoezi la kupiga kura Lubumbashi, Novemba 2011 (Picha ya kumbukumbua).
Zoezi la kupiga kura Lubumbashi, Novemba 2011 (Picha ya kumbukumbua). AFP PHOTO/PHIL MOORE

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupitia waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo imesema kuwa raia wa DRC waishio ugenini hawatoshirikishwa katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mnamo mwezi Desemba mwaka huu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mambo ya Nje Emmanuel Ilunga, ameiambia RFI kwamba muswada wa sheria kuhusiana na hatua hiyo utawasilishwa bungeni ili kupitishwa.

Waziri Ilunga ameelezea kwa nini, kwa mujibu wa serikali, raia wa DRC waishio ugenini hawataweza kupiga kura licha ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo mara mbili.

"Ni gharama ya kifedha ya uchaguzi huo na matatizo ya vifaa ambayo inaelezea hatua hiyo, " amesema Bw Ilunga.

"Uchaguzi utafanyika, lakini kwa bahati mbaya, kwa maoni yangu, raia waishio ugenini hawatoshiriki uchaguzi huo ... wako nje ya nchi na hakutakuwa na kituo cha kupigia kura nje ya nchi. Wale ambao wanataka kupiga kura wanaweza kuja nchini, kuchukua kadi na kurudi kupiga kura nchini hapa, " ameongeza waziri wa mambo ya nje wa DRC.

Haiwezekani, hadi mwezi Desemba, tarehe ya uchaguzi, kuandaa uchaguzi katika nchi 180 wanakoishi raia wa DRC, waziri Ilunga amesema.

"Ikiwa tunataka kujiunga na nchi zote duniani haitawezekana hadi kufikia mwezi Desemba ... Kwa sababu kuna nchi 180. Kwa hivyo tunapaswa kwenda kila nchi, kama jinsi sheria inasema. Na kwa muda huu haiwezekani. Kwa hiyo ikunahitajika muda wa kutosha, kunahitajika maandalizi ya kutosha,kunahitajika vifaa na na yote hayo yanaendana na fedha.Eleweni kwamba tatizo za kifedha zipo. Ni kweli".