MOROCCO-HAKI

Viongozi wa maandamano wahukumiwa kifungo cha miaka 20 Morocco

Katika Mahakama ya Casablanca ambapo kesi ya viongozi wa kundi la Hirak imekua ikisikilizwa.
Katika Mahakama ya Casablanca ambapo kesi ya viongozi wa kundi la Hirak imekua ikisikilizwa. FADEL SENNA / AFP

Viongozi wa kundi la "Hirak", lilohamasisha maandamano ya kijamii yaliyoitikisa Morocco mnamo mwaka 2016 na 2017, wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, kufuatia kesi tata iliyodumu miezi tisa. Uamuzi huo ulitolewa Jumanne jioni wiki hii na Mahakama ya Casablanca.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa kundi hilo, Nasser Zefzafi na viongozi wengine watatu, Nabil Ahmjiq, Ouassim Boustati na Samir Ighid, wamepewa adhabu kubwa kutokana na "njama kuhatarisha usalama wa nchi," mashtaka ambayo yanaweza kuendana na adhabu ya kifo kulinagana na uamuzi huo.

Jumla ya watu 53 walisikilizwa katika kesi hiyo. Adhabu ndogo katika kesi hiyo ni ya mwaka mmoja gerezani, na kulipa faini ya Dirham 5,000 (sawa na Euro 450), kwa mujibu wa uamuzi wa uliyotolewa na Kitengo cha Jinai katika Mahakama ya Rufaa ya Casablanca. Watuhumiwa hawakuepo wakati uamuzi huo ulitolewa.

Watuhumiwa wengine watatu, Mohamed Haki, Zakaria Adehchour na Mahmoud Bouhenoud wamepewa kifungo cha miaka 15 jela, miaka 7 hadi 10 jela, pia kutokana na "njama za kuhatarisha usalama wa nchini."

Wanasheria wa watuhumiwa wameikosoa serikali kuishinikiza mahakama kuchukua uamuzi, wakisema kwamba serikali imeshindwa katika mtihani wa kuheshimu haki za binadamu na uhuru kwa vyombo vya sheria.