DRC-KABILA-SIASA-USALAMA

DRC yafanya mabadiliko katika jeshi lake

Askari wa jeshi laDRC wakipiga doria huko Rwangoma, mji wa mashariki mwa DRC, mwezi Agosti 2016.
Askari wa jeshi laDRC wakipiga doria huko Rwangoma, mji wa mashariki mwa DRC, mwezi Agosti 2016. © Sonia Rolley / RFI

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefanya mabadiliko makubwa katika jeshi lake, ikiwa imesalia miezi isiyozidi minne kabla ya Uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 23. 

Matangazo ya kibiashara

Siku chache zilizopita, rais Joseph Kabila Kabange alifanya mabadiliko kwenye ngazi za uongozi wa jeshi la DRC, FARDC.

Zoezi hilo limeendelea kushika kasi ambapo Jumanne wiki hii, serikali ilitangaza kuanza kwa zoezi hilo ambalo litahusu jeshi lote la DRC. Kanda zote za ulinzi zinahusika kwa zoezi hilo, serikali imesema.

Mkuu wa kanda ya kwanza ya ulinzi ambayo makao yake makuu ni mjini Kinshasa, ni Jenerali Fall Sikabwe Asinda anachukua nafasi ya Jenerali Gabriel Amisi Kumba, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa majeshi anayehusika na Operesheni na Upelelezi. Jina la Fall Sikabwe Asinda linajulikana sana kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Monusco. Mnamo mwaka 2015, uteuzi wake kama mkuu wa majeshi katika mkoa wa Kivu ulizua mvutano mkubwa na Monusco na kusababisha kusitishwa kwa ushirikiano kati ya ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini humo na jeshi la DRC. Wakati huo, Umoja wa Mataifa uliona kuwa hauwezi kushirikiana na Jenerali huyo, anayeshtumiwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hali hiyo ilidumu zaidi ya mwaka.

Jenerali Jean-Claude Kifwa, anaondoka Lubumbashi na ameteuliwa kuwa mkuu kambi ya kijeshi ya Kamina. Kanda ya tatu la ulinzi itaongozwa kwa sasa na Jenerali Constant Ndima Kongba.

Wakati ambapo kunazungumziwa kurudi kwa mwanasiasa mkuu wa upinzani Jean-Pierre Bemba, katika mkoa anakotoka wa Equateur, ametuliwa Jenerali Eric Ruhorimbere, ambaye hivi karibuni aliwekwa chini ya vikwazo. Eric Ruhorimbere anashukiwa kwa miaka ishirini kujihusisha na mauaji ya raia mashariki mwa DRC. Lakini pia anashtumiwa kuhusika katika mauaji yaliyotokea Kasaï na hivyo kuchukuliwa vikwazo na jumuiya ya kimataifa.

Majina mengine kwenye Orodha Nyekundu ya Umoja wa Mataifa, ni pamoja na Majenerali Muhindo Akili Mundos na Muhima Dieudonné. Wote wawili wanashutumiwa na kundi la wataalamu kujihusisha na biashara haramu ya silaha na miti katika eneo la Beni. Wameteuliwa kuongoza vikosi vya askari katika mkoa wa Kivu Kusini.

Jenerali Philemon Yav, mshirika wa karibu wa Joseph Kabila, ameteuliwa kuwa mkuu wa majeshi katika kanda ya pili ya ulinzi. Jenerali Philemon, hapo awali alishtumiwa kujihusisha na biashara haramu ya silaha na waasi mnamo mwaka 2007. Wataalam wa Umoja wa Mataifa walimshtumu kuwapa silaha waasi wa Kihutu wa Rwanda (FDLR).

Wadadisi wanasema Joseph Kabila ameanza kuimarisha safu yake katika jeshi kwa minajili ya kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika jeshi na taasisi zingine za nchi.