ZIMBABWE-EU-UCHAGUZI-SIASA

Umoja wa Ulaya kutoa ripoti yake kuhusu uchaguzi Zimbabwe

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya (EU) wanatarajia kutoa ripoti yao Jumatano wiki hii kuhusu uchaguzi wa urais nchini Zimbabwe, wakati ambapo wananchi wanaendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi.

Moja ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa urais Zimbabwe, Julai 30,  2018.
Moja ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa urais Zimbabwe, Julai 30, 2018. RFI/Alexandra Brangeon
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa vyanzo rasmi, matokeo ya uchaguzi wa urais yatatangazwa siku ya Ijumaa au Jumamosi wiki hii.

Tayari Upinzani umedai kuwa mgombea wao Nelson Chamisa ameshinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo wa urais dhidi ya rais anayemaliza muda wake Emmerson Mnangagwa.

Wakati huo huo Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe imetangaza kwamba chama cha Rais Emmerson Mnangagwa, Zanu-PF kimepata viti vingi bungeni.

Tamko hili la upinzani limeichukiza serikali ambayo imetishia kuwafunga wale wanaotangaza matokeo wakati ambapo zoezi la kuhesabu linaendelea kuchelewa.

MDC inaitaka Tume ya Uchaguzi kutangaza mshindi wa Uchaguzi huo, huku kikidai kuwa, chama tawala ZANU PF kinapanga kuiba kura.

Tendai Biti mmoja wa viongozi wa juu wa MDC nchini humo amewaambia wanahabari jijini Harare kuwa, chama chake kina uhakika wa ushindi lakini wana hofu ya wizi wa kura.

Awali, rais Emmerson Mnangagwa na kiongozi mkuu wa upinzani Nelson Chamisa, wote walidai kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda Uchaguzi huo.

Huu umekuwa ni Uchaguzi wa kwanza, kufanyika bila ya kuwepo kwa rais wa zamani Robert Mugabe ambaye aliondolewa madarakani mwaka 2017, baada ya kuwa madarakani tangu mwaka 1980.