ZIMBABWE-UN-EU-SIASA-USALAMA

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya walaani machafuko Zimbabwe

Katika kituo cha kupigia kura huko Chegutu, Zimbabwe, tarehe 30 Julai 2018.
Katika kituo cha kupigia kura huko Chegutu, Zimbabwe, tarehe 30 Julai 2018. REUTERS/Philimon Bulawayo

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kwa pamoja wanashtumu vikosi vya usalama vya Zimbabwe kutumia nguvu kupita kiasia dhidi ya waandamanaji wa upinzani ambao waliingia mitaani siku ya Jumatano kupinga kile walichosema chama tawala cha Zanu-PF kinajaribu kufanya udanganyifu ili kumruhusu Emmerson Mnangagwa kushinda.

Matangazo ya kibiashara

Ghasia zimezuka nchini Zimbabwe kati ya wafuasi wa upinzani na vikosi vya usalama katika mji mkuu wa Zimbabwe huku kukiwa na maandamano dhidi ya kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi

Mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Maandamano hayo ya wafuasi wa chama cha upizani cha MDC mjini Harare yalibadilika na kuwa mabaya nyakati za mchana.

Matokeo yanaonyesha kwamba Zanu-PF inashinda viti vingi vya ubunge katika uchaguzi huo tangu kung'atuliwa madarakani kwa Robert Mugabe.

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe (ZEC) imetangaza kwamba Zanu-PF kufikia sasa imejishindia viti 110 huku MDC ikijipatia viti 41 kulingana na chombo cha habari cha ZBC.

Kuna viti 210 katika bunge la taifa hilo.

Upinzani nchini Zimbabwe unasema kuwa mgombea wake wa urais Nelson Chamisa, ameshinda uchaguzi mkuu wa Jumatatu.

Chama cha upinzani cha MDC kinasema kuwa chama tawala cha Zanu-PF kinajaribu kufanya udanganyifu ili kumruhusu Emmerson Mnangagwa kushinda , na kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo hakutakubalika.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa hakuna udanganyifu na inahitaji muda ili kuhesabu kura hizo.

Mapema, chama cha upinzani cha MDC kilikuwa kimesema kwamba kura hiyo ilifanyiwa udanganyifu na kwamba mgombea wake Nelson Chamisa alikuwa ameibuka mshindi.

Umoja wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo.

Wakati huo huo Umoja wa Afrika umesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki, ukiongezea kuwa unaadhimisha wakati muhimu wa mabadiliko ya kisiasa.

Ripoti ya awali kutoka waangalizi wa SADC inasema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa amani na ulifanyika kulingana na sheria.

Matokeo ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutangazwa Ijumaa wiki hii. Lakini Umoja wa Mataifa umetaka matokeo hayo yatangazwe haraka iwezekanavyo ili kuepuka na machafuko zaidi.

Zanu-PF ambacho kimekuwa madarakani tangu 1980 kimeshutumiwa kufanya udanganyifu katika miaka ya nyuma ili kumweka Mugabe madarakani.