DRC-KATUMBI-SIASA-HAKI

Moise Katumbi apinga marufuku ya kutua Lubumbashi

Moise Katumbi mnamo Juni 2015.
Moise Katumbi mnamo Juni 2015. FEDERICO SCOPPA / AFP

Mamlaka nchini DRC imetoa taarifa rasmi kwa Moise Katumbi, mwanasiasa wa upinzani aliye uhamishoni kwamba wamekataa kurudi kwake nchini DRC. Moise Katumbi anatarajia kurudi nyumbani Ijumaa hii, Agosti 3.

Matangazo ya kibiashara

Gavana wa zamani wa Katanga alikua alipanga kurudi nchini akipitia Lubumbashi ili kuchukua fomu ya kuwania katika uchaguzi wa urais, lakini hajapewa ruhusa ya ndege yake kutua katika ardhi ya DRC. Hata hivyo Moise Katumbi na washirika wake wanaonekana kupuuzia marufuku hiyo.

Moise Katumbi alitangaza kwamba atawasili Lubumbashi Ijumaa asubuhi, Agosti 3, lakini ndege yake binafsi haijapewa ruhusa ya kutua. Katika barua, meya wa Lubumbashi, Ghislain Robert Lubaba Buluma amesema ndege hiyo imekataliwa kutua au kupaa katika anga ya DRC pamoja na mashitaka yanayoendelea kumkabili Moise Katumbi.

Siku ya Alhamisi, ofisi ya mashitaka ilitangaza kwamba Moise Katumbi atakamatwa baada ya kuwasili nchini DRC kwa kosa la kuhatarisha usalama wa taifa. "Moise Katumbi anakabiliwa na mashitaka ya kuajiri askari mamluki kwa lengo la kuangusha utawala wa rais Joseph Kabila", vyanzo kadhaa vya serikali vimebaini.

Wanasheria wake wanasema wanashangazwa na mwenendo huo wa ofisi ya mashitaka. Kesi hiyo, kwa mujibu wa wanasheria wake, ilikuwa ikisubiriwa kusikilizwa baada ya kukataa rufaa. Wanasheria hao wanasema "ofisi ya mashitaka imeharakia kutangaza hatua hiyo wakati ambapo hakuna sababu ya mteja wao kukamatwa.

"Tumesikia kuhusu tishio hili la kukamatwa. Tuko katika nchi ya sheria, kukamatwa kunaendana kulingana na sheria na utaratibu, " amesema Jean-Joseph Mukendi, mratibu wa muungano wa wanasheria wa Katumbi.

Moise Katumbi anataka kurudi DRC ili kuchukua fomu ya kuwania katika uchaguzi wa uraisa wa Desemba 23, 2018.