DRC-SIASA-USALAMA

Joseph Kabila aitisha washirika wake kuchagua mgombea

Rais wa DRC Joseph Kabila ameitisha kikao na wajumbe wa vyama vinavyomuunga mkono. Ajenda ya mkutano huo ni uteuzi wa mgombea urais katika uchaguzi wa Agosti 8, siku moja kabla ya muda uliyotolewa kwa wagombea kuwasilisha fomu zao kumalizika, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Rais wa DRC Joseph Kabila katika kikao maalum cha Bunge baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Augustin Matata, Novemba 15, 2016.
Rais wa DRC Joseph Kabila katika kikao maalum cha Bunge baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Augustin Matata, Novemba 15, 2016. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Katiba, rais Kabila hawezi kuwania katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Desemba 23, lakini hadi sasa amesalia kimya kuhusu uteuzi wa mtu atakayepeperusha bendera ya chama tawala cha PPRD na washirika wake .

"Washirika wote waliotia saini mkataba wa kuundwa kwa muungano wa vyama vinavyounga mkono serikali (FCC) wanakutana leo jioni katika mkutano muhimu huko Kingakati, " waziri ambaye hakutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP.

“Sio siri tena, itakuwa suala la uteuzi wa mgombea ambaye atapeperusha bendera ya muungano wetu katika uchaguzi wa urais," ameongeza shirika mwingine wa karibu na rais Kabila ambaye pia hakutaja jina lake.

DRC ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi Afrika licha ya rasilimali zake,haijawahi kushuhudia mchakato wa kupeana madaraka kwa amani tangu kupata uhuru kutoka mikononi mwa Ubelgiji Juni 30, 1960.