DRC-SIASA-USALAMA

Ramazani Shadary kupeperusha bendera ya PPRD na washirika wake DRC

Rais wa DRC Joseph Kabila.
Rais wa DRC Joseph Kabila. REUTERS/Kenny Katombe/File Photo

Rais wa DRC Joseph Kabila hatowania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23. Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, ameteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha PPRD na washirika wake.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa kwanza wa sasa wa chama cha rais cha PPRD, Emmanuel Ramazani Shadary anatarajiwa kuwasilisha fomu yake kwenye Tume ya Uchauzi (CENI) ikiwa zimesalia saa chache kabla ya kumalizika muda wa wagombea urais kuwasilisha fomu zao za kuwania uchaguzi wa Desemba 23, msemaji wa serikali Lambert Mende amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

Uamuzi huo umetolewa baada ya mkutano wa saa mbili, mkutano ulioitishwa tangu siku ya Jumanne wiki hii na rais Joseph Kabila.

Katika mkutano huo wajumbe wamekubaliana kwamba rais Joseph Kabila hatowania uchaguzi wa Desemba 23 DRC .

Kwa mujibu wa Katiba ya DRC, rais Joseph Kabila hastahili kuwania tena katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23.

DRC ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi Afrika licha ya rasilimali zake, haijawahi kushuhudia mchakato wa kupeana madaraka kwa amani tangu kupata uhuru wake kutoka mikononi mwa Ubelgiji Juni 30, 1960.