ZIMBABWE-SIASA-UCHAGUZI-HAKI

MDC yawasilisha mahakamani kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Zimbabwe

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimewasilisha kesi Mahakamani kupinga ushindi wa rais Emmerson Mnangangwa wakati huu mmoja wa kiongozi wake Tendai Biti akikimbilia nchini Zambia.

Kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa katika mkutano na waandishi wa habari Agosti 3, Harare.
Kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa katika mkutano na waandishi wa habari Agosti 3, Harare. REUTERS/Mike Hutchings
Matangazo ya kibiashara

Upinzani nchini humo unasema Tume ya Uchaguzi ilimsaidia Mnangangwa kupata ushindi, na kura za mgombea wake Nelson Chamisa ziliibiwa.

Wakili wa upinzani Thabani Mpofu, amesema tayari upinzani umeandaa ushahidi wa kutosha kuonesha namna kura zilivyoibiwa, uko tayari kupambana na Tume ya Uchaguzi katika Mahakama hiyo ya Kikatiba.

Wakati huo huo, mmoja wa viongozi wa juu wa upinzani Tendai Biti amekimbilia nchini Zambia, alikoomba hifadhi ya kisiasa baada ya serikali kuanza msako dhidi ya wapinzani wanaodaiwa kusababisha machafuko wiki iliyopita jijini Harare.

Hata hivyo, kumekuwa na ripoti za kukanganya kuhusu aliko Bwana Biti, huku wengine wakisema amezuiwa mpakani lakini chama chake kinasema tayari yupo jijini Lusaka.

Waziri wa Mambo ya nje wa Zambia Joe Malanji ameiambia BBC kuwa, Biti amenyimwa hifadhi hiyo kwa sababu serikali haikuridhika na sababu zake, lakini yupo salama nchini humo na atarejea nchini mwake hali itakapotulia.