DRC-EBOLA-AFYA

Kumi wafariki kutokana na maambukizi ya Ebola DRC

Virusi vya Ebola.
Virusi vya Ebola. CDC/Frederick A. Murphy

Mlipuko mpya wa ugonjwa hatari wa Ebola umeua watu 10 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na ripoti mpya iliyochapishwa na Wizara ya Afya.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, mamlaka ya afya ya DRC wameanza kuchunguza sababu za vifo vya watu wengine 27 ili kujua ikiwa wameambukizwa virusi vya Ebola.

Hata hivyo, mamlaka imeripoti kesi nyingine 54 ambazo zinafanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Mlipuko huu wa kumi wa ugonjwa hatari wa Ebola nchini DRC ulizuka tarehe 1 Agosti karibu na mji wa Beni, mashariki mwa DR Congo. Ugonjwa huu hatari umeathiri eneo lenye "usalama duni" kutokana na kuwepo kwa makundi mengi ya watu wenye silaha kutoka nchi za kigeni na yale yanayoundwa na raia wa nchi hiyo.

Chanjo dhidi ya ugonjwa huo ilianza Jumatano katika eneo lililoathiriwa. Dk. Richard Kitenge, Mkuu wa Taifa wa Huduma ya Matibabu, amewasili Goma kusaidia viongozi wa afya za katika mji huo "kuweka mpango maalum" ikiwa ugonjwa wa Ebola utaripotiwa katika mji huo ulio kwenye mpaka na Rwanda.

Watu wa Goma wamehamasishwa kuhusu njia za kuzuia ugonjwa wa Ebola.