NIGERIA-USALAMA-MAUAJI

Kumi wauawa katika shambulizi la watu wenye silaha Nigeria

Watu wenye silaha wameua watu kumi, ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi, wakati wa shambulio kwenye kituo cha polisi na benki mbili kusini mwa Nigeria, polisi imesema leo Ijumaa.

Polisi wa Nigeria wakipiga doria.
Polisi wa Nigeria wakipiga doria. REUTERS/Austin Ekeinde
Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji walishambulia kwanza kituo cha polisi kwa lengo la kuiba silaha, kabla ya kufanya shambulio jingine katika benki mbili siku ya Alhamisi huko Igarra, katika Jimbo la Edo, chanzo hicho kimesema.

"Kwa jumla, watu kumi waliuawa. Wahalifu walishambulia kwanza kituo cha polisi ambapo waliuawa watu watatu, ikiwa ni pamoja na wafungwa wawili na afisa wa polisi," afisa wa polisi ambaye hakutaja jina lake, ameliambia shirika la habari la AFP.

Watu watatu karibu na kituo cha polisi pia walipoteza maisha baada ya kutawa na risasi hewa, pamoja na watu wanne, ikiwa ni pamoja na wateja katika benki mbili, ameongeza.

"Wezi walishambulia benki mbili lakini hawakuweza kuiba fedha," amesema.

Msemaji wa polisi wa Edo, Chidi Nwabuzor amethibitisha mashambulizi hayo, lakini alikataa kutoa habari zaidi.

Kiongozi wa jumii ya Folorunsho Dania pia amesema kuwa watu 10 waliuawa. "Hili ni tukio baya," ameviambia vyombo vya habari vya Nigeria.

“Miili kumi imehesabiwa, kituo cha polisi kilichomwa moto, gari la mkuu wa polisi katika eneo pia lilichomwa moto," ameongeza.