ZIMBABWE-BITI-SIASA-USALAMA-HAKI

Mnangagwa: Biti ameachiliwa huru baada ya mimi kuingilia kati

Mataifa ya Magharibi na Umoja wa Mataifa, yameshutumu kufukuzwa nchini Zambia na kufikishwa Mahakamani mmoja wa viongozi wa juu wa upinzani nchini Zimbabwe Tendai Biti..

Tendai Biti akifikishwa mahakamani, Harare Agosti 9, 2018.
Tendai Biti akifikishwa mahakamani, Harare Agosti 9, 2018. Jekesai NJIKIZANA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Biti alikamatwa baada ya kufukuzwa nchini Zambia siku ya Alhamisi wiki hii na kufikishwa Mahakamani jijini Harare akiwa amefungwa pingu na kushtakiwa kwa uchochezi wa maandamano ya kisiasa wiki iliyopita, kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mshindi wa kiti cha urais.

Mwanasiasa huyo amekanusha madai hayo lakini ameachiliwa kwa dhamana baada ya kutoa Dola elfu tano na kuagizwa kuleta pasi yake ya kusafiria Mahakamani pamoja na kutohotubia mikutano ya kisiasa na kuzungumza na wanahabari.

Rais Emmerson Mwanangwa kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema yeye ndio aliyesaidia Bwana Biti kuachiliwa huru.

Kiongozi huyo wa Zimbabwe ametaka kuwepo kwa amani. Lakini amesisitiza kuwa taratibu zaidi za kisheria zitafuata mkondo wake.