CAMEROON-MAUAJI-USALAMA

Cameroon kuchunguza video mpya ya mauaji

Jeshi la Cameroon laendelea kushtumiwa kwamba limekua likitekeleza mauaji katika maene mbalimbali kaskazini mwa nchi hiyo.
Jeshi la Cameroon laendelea kushtumiwa kwamba limekua likitekeleza mauaji katika maene mbalimbali kaskazini mwa nchi hiyo. RFI/OR

Msemaji wa serikali ya Cameroon, Issa Bakary Tchiroma, ameahidi kwamba uchunguzi utaanzishwa kuhusu video mpya iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inaonyesha mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na jeshi katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa redio ya serikali.

Matangazo ya kibiashara

Video hiyo ambayo ilirekodiwa kabla ya mwezi Mei 2016 kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amesty International na ambayo ilirushwa hewani mapema mwezi Agosti, inaonyesha watu wenye silaha wakiwafyatulia risasi watu kadhaa wasiokuwa na silaha karibu na ukuta wa nyumba iliyokua ikiungua.

Video hii "itafanyiwa uchunguzi wa kina, uchunguzi ambao utaagizwa na Mkuu wa Nchi" Paul Biya, ameahidi Bw Tchiroma, Waziri wa Mawasiliano, katika mahojiano na redio ya serikali. Amesema kuwa waandishi wa habari watapewa taarifa kuhusu matokeo ya uchunguzi.

Hata hivyo, "amefutilia mbali" taarifa zinazosema kuwa askari wa Cameroon walihusika na mauaji hayo.

"Tusubiri matokeo ya uchunguzi ili kubaini chanzo na sababu mauaji hayo na waliohusika ili waweze kuchukuliwa hatua, " amesema Waziri wa Habari wa Cameroon na msemaji wa serikali, Issa Bakary Tchiroma.

Katika video hii, askari moja anayedaiwa kuwa ni wa jeshi la Cameroon anabaini kwamba yuko katika operesheni ya kuwatafuta maadui wa nchi katika kijiji cha Achigachia, kwenye mpaka na Nigeria.

Kati ya mwaka 2014 na 2016, Achigachia ilikua mmoja ya maeneo yaliyo kabiliwa kwa mara kadhaa na mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram. Vita vingi kati ya jeshi la Cameroon na Boko Haram vilitokea katika eneo hilo.

Leo kuna utulivu katika mji huo, video hiyo inaweza kuwa ilirekodiwa wakati huo wa vita, kwa mujibu wa Amnesty International.