Mwili wa Jonas Savimbi kufukuliwa na kuzikwa kwa heshima Angola
Imechapishwa:
Chama cha Unita nchini Angola kimetangaza kwamba mwili wa aliyekuwa kiongozi wa waasi wa Unita kabla haijasajiliwa kuwa chama cha siasa nchini humo, Jonas Savimbi, utafukuliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu na kuzikwa kwa heshima, kwa mujibu wa chama shirika la habari la AFP.
Kiongozi wa sasa wa chama cha Unita Isaias Samakuva, ametangaza kuwa mwili wa Savimbi utafukuliwa na kisha uzikwe upya kwa heshima kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kauli hii aliitoa baada ya kukutana na rais JJoao Lourenço katika mji mkuu Luanda siku ya Jumatano.
Mapema mwezi huu Bw Samakuva aliilaumu serikali kwa kumnyima Savimbi maziko Mazuri.
Savimbi aliuawa na vikosi vya serikali tarehe 22 Februari mwaka 2002 na kuzikwa siku iliyofuatia karibu na eneo alipouawa katika mkoa wa Moxico, mashariki mwa Angola.
Wiki sita baadaye Unita walisaini makubaliano ya amani na serikali na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 27.
Jonas Savimbi aliliongoza kundi hili la waasi wa Unita kwa miaka mingi kabla ya kusajiliwa kuwa chama cha kisiasa, baada ya kifo chake.