NIGERIA-MAUAJI-USALAMA

Watoto zaidi ya 33 wafariki dunia katika kambi Nigeria

Mji wa Bama (kaskazini mashariki mwa Nigeria), Desemba 8, 2016, baada ya kundi la Boko Haram kutimuliwa, umeanza kukarabatiwa.
Mji wa Bama (kaskazini mashariki mwa Nigeria), Desemba 8, 2016, baada ya kundi la Boko Haram kutimuliwa, umeanza kukarabatiwa. STEFAN HEUNIS / AFP

Watoto wasiopungua 33 walifariki ndani ya kipindi cha wiki mbili kati ya tarehe 2 na 15 Agosti katika kambi moja kaskazini mwa Nigeria, ambako wanaishi watu waliofukuzwa makwao kufuatia kuzuka kwa uasi wa kundi la Boko Haram, Shirika la MSF limebaini leo Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema kuwa limeweka mpango wa misaada ya dharura kwa wakimbizi wa kambi hiyo, ilioko Bama, zamani mji wa pili wa jimbo la Borno, ambao umekua sasa kituo cha shughuli za kibidamu.

"Watoto wengi wako katika hali mbaya wanapowasili katika kambi ya Bama, na hali yao inaendelea kuwa mbaya zaidi katika kambi kwa kukosa msaada na huduma," MSF imesema katika taarifa yake.

"Wanafariki kwa utapiamlo," amesema Lisa Veran, msemaji wa MSF mjini Paris.

Tangu mwezi Aprili 2018, zaidi ya watu 10,000 wamewasili Bama, MSF imesema.

"Misaada iliyotolewa haitoshi kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wanaoendelea kuwasili kila kukicha. Kambi hiyo, iliyojengwa kwa kuwapokea watu 25,000, imejaa tangu mwishoni mwa mwezi Julai," MSF imeongeza.

Mnamo mwezi Juni, krais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambaye hivi karibuni alitangaza kuwa atawania katika uchaguzi wa urais, alisema kuwa eneo la kaskazini-mashariki liko katika "hatua ya kurejea kwa amani baada ya machafuko".

Lakini ongezeko la mashambulizi ya hivi karibuni lilisababisha mdororo wa usalama katika eneo hilo. Askari walikaidi amri ya serikali ya kupambana katika eneo linalodhibitiwa na Boko Haram, baada ya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi yaliyosababisha vifo vingi upande wa askari katika miezi ya hivi karibuni.