AFRIKA KUSINI-ZUMA-UCHUMI

Maafisa kadhaa wa serkali kuchunguzwa kuhusu rushwa Afrika Kusini

Tume maalum kutoka idara ya Mahakama nchini Afrika Kusini, inaanza leo kuchunguza madai ya ufisadi yanayowahusisha maafisa wa juu wa serikali.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma wakati wa kesi yake, akiongozana na mwakilishi wa kampuni ya Thales Christine Guerrier huko Durban tarehe 6 Aprili 2018.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma wakati wa kesi yake, akiongozana na mwakilishi wa kampuni ya Thales Christine Guerrier huko Durban tarehe 6 Aprili 2018. Nic Bothma/Pool via Reuters
Matangazo ya kibiashara

Uchunguzi huu utakuwa wa wazi na utaongozwa na Naibu Jaji Mkuu Raymond Zondo, huku wale wanaolengwa wakiwa ni maafisa walioshiriki katika serikali ya zamani ya rais Jacob Zuma.

Tume hiyo haina uwezo wa kumkamata mshukiwa au kumfungulia mashataka lakini, ushahidi utakapopatikana unaweza kutumiwa katika kesi za ufisadi Mahakamani, katika siku zijazo.

Hivi karibuni Mahakama ya Afrika Kusini iliahirisha kwa mara nyingine kesi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jacob Zuma hadi Novemba 30. Jacob Zuma anashtumiwa kashfa ya rushwa katika mkataba wa silaha. Kesi hiyo iliahirishwa ili kuwezesha wanasheria wake wapya kufahamu yaliomo katika kesi inayomkabili mteja wao.

Zuma, mwenye umri wa miaka 76, anashutumiwa kuwa alipokea rushwa kutoka kwa kampuni ya elektroniki na ulinzi Thales katika mkataba wa silaha wenye thamani ya karibu euro bilioni 4 uliyotolewa mwaka 1999.

Jacob Zuma, wakati huo "waziri" wa serikali ya mkoa kisha makamu wa rais wa Afrika Kusini, amekanusha shutma hizo dhidi yake.

Kampuni ya Ufaransa Thales pia imehusishwa katika kesi hiyo.

Mwanasheria wa "Kihistoria" wa Jacob Zuma, Michael Hulley, hivi karibuni alijiondoa kwenye kesi hiyo kwa sababu ya utata kuhusu malipo ya ada yanayohusiana na utaratibu wa mahakama kwa mteja wake ambayo yalitakiwa kulipwa na serikali. Swala ambalo linapaswa kutatuliwa hivi karibuni na mahakama.