DRC-SIASA-USALAMA

Rais wa Seneti DRC: Mimi naunga mkono kurejea kwa Katumbi

Spika wa Bunge la Seneti DRC Léon Kengo Wa Dondo.
Spika wa Bunge la Seneti DRC Léon Kengo Wa Dondo. DR

Spika wa Baraza la Seneti nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Leon Kengo wa Dondo ameitaka serikali ya nchi hiyo kuhakikisha mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi anarejea nchini na kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka huu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Akihojiwa na mwandishi wa RFI Idhaa ya kifaransa Florence Morice, aliyeko jijini Kinshasa, Leon Kengo amesema nchi ya DRC imefika katika kipindi cha kuonyesha ulimwengu kuwa ni nchi ya kidemokrasia.

Serikali ya DRC inaendelea kushinikizwa kumruhusu mwanasiasa na gavana wa zamanani wa mkoa wa zamani wa Katanga Moise Katumbi Chapwe kurejea nchini.

Hivi karibuni Moise Katumbi Chapwe alijaribu mara kadhaa bila mafanikio kuingia nchini DRC akipitia Zambia.

Serikali ya DRC kupitia msemaji wake Lambert Mende anasema Moise Katumbi anakabiliwa na mashtaka ya kuhatarisha usalama wa taifa. Madai ambayo Bw Katumbi na wanasheria wake wanafutilia mbali na kudai kuwa kesi yake ni ya kisiasa.