MOROCCO-HAKI-USALAMA-SIASA

Mohammed VI atoa msamaha kwa wanaharakati wa Hirak

Maandamano ya kuunga mkono vuguvugu la Hirak huko Rabat, Morocco, Juni 27, 2018.
Maandamano ya kuunga mkono vuguvugu la Hirak huko Rabat, Morocco, Juni 27, 2018. © REUTERS/Youssef Boudlal

Mfalme wa Morocco Mohamed wa 6 ametoa msamaha kwa wafungwa 889, ikiwa ni pamoja na wafungwa 160 waliohusika katika maandamano yaliyoitishwa na vuguvugu la Hirak katika Jimbo la Rif mnamo mwaka 2016 na 2017.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo ulichukuliwa siku ya Jumanne wiki hii wakati wa kusheherekea Eid El-Adha, sikukuu kubwa ya Kiislam.

Kulingana na taarifa za RFI, karibu watu 100 tayari wametoka gerezani huko Casablanca, Fez au Al Hoceima, eneo ambako maandamano makubwa yalishuhudiwa.

Mnamo mwezi Oktoba 2016, kifo cha mfanyabiashara wa samaki aliyegongwa na lori la kubeba uchafu kilichochea vurugu katika Jimbo hilo. Hali hiyo ilitokea wakati ambapo raia wa eneo hilo lililo kaskazini mwa Morocco, walikua bado na hasira ya kutengwa kwa jimbo lao na utawala wa kifalme wa nchi hiyo.

Kwa upande wa mmoja wa wanasheria wa vuguvugu la Hirak na kiongozi wa vuguvugu hilo Nasser Zefzafi, wanasema hatua hiyo ya Mfalme Mohamed VI inaonyesha mabadiliko ya mtazamo kwa upande wa mamlaka ya kifalme.

"Utawala huu wa Alawite, ikiwa ni pamoja na Mohammed VI au baba yake Hassan II, hauna tabia ya kuwasamehe wale wanaochukuliwa kuwa ni waasi," amesema wakili Mohamed Zayan. Hivyo hatua hii ya Mohammed VI ya kuwasamehe, watu hao, hata kama haitoshi, inatosha kwa kiasi fulani kuamini kwamba kuna njia mpya kuhusu suala hili. "

Bw Zayan anaamini kwamba utawala unataka kupunguza mvutano unaoendelea katika jimbo hilo.