MSUMBIJI-VYOMBO VYA HABARI

HRW: Msumbiji inatoza kodi kubwa kwa vyombo vya habari

Maputo, mji mkuu wa Msumbiji.
Maputo, mji mkuu wa Msumbiji. Wikimedia

Msumbiji imetangaza ongezeko kubwa la ada linalotozwa kwa wanahabari wanaotaka kufanya kazi nchini humo hasa wale wa kigeni. Hatua hii imeshtumiwa vikali na Mashirika ya kutetea haki za Binadmau na kuelezwa kama uvunjifu mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari.

Matangazo ya kibiashara

Wanahabari wa kigeni wanaoishi nchini humo watatakiwa kulipa Dola 8,600 kwa mwaka ili kuruhusiwa kufanya kazi huku wale wanaotembelea nchi hiyo wakihitaji kulipa Dola 1,700.

Sheria hii iliyopitishwa katika baraza la mawaziri mwezi uliopita kwa lengo rasmi la kusimamia vizuri uendeshaji kazi wa vyombo vya habari,ilianza kutumika Jumatano wiki hii, ikiwa imesalia miezi miwili tu kabla ya uchaguzi.

Ongezeko hili la ghafla limekua ni mzigo mkubwa kwa vyombo vya habari vya nchini humo. Kodi inayotakiwa na mamlaka ili kusajili kituo cha televisheni imeongezeka hadi euro 45,000.

Shirika linalotetea haki ya vyombo vya habari nchini Msumbiji, MISA, limetangaza nia yake ya kuwasilisha malalamiko yake mbele ya mahakama.

"Sheria hii ni kinyume na Katiba ya nchi na sio halali, lengo letu sisi ni kufutwa kwa sheria hiyo," amesema kiongozi wa MISA, Ernesto Nhanale.

Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Right Watch limesema limeshtumu "kushindwa kupatikana kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Msumbiji," huku Amnesty International ikipinga "jaribio la wazi la kuwakandamiza waandishi wa habari."