DRC-SIASA-USALAMA

Tume ya Uchaguzi kutangaza majina ya wagombea urais DRC

Orodha ya muda ya wagombea urais na katika uchaguzi wa wabunge katika ngazi ya kitaifa wa Desemba 23 nchini DRC itajulikana Ijumaa hii, Agosti 24, kwa mujibu wa vyanzo kutoka Tume ya Uchaguzi, CENI.

Chama cha Jean-Pierre Bemba, hapa wakati akiwasilisha fomu ya kuwania katika uchaguzi wa urais, Kinshasa, Agosti 2, 2018, kinasema kina wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokuwepo kwa mgombea wake kwenye orodha iliyochapishwa na Ceni.
Chama cha Jean-Pierre Bemba, hapa wakati akiwasilisha fomu ya kuwania katika uchaguzi wa urais, Kinshasa, Agosti 2, 2018, kinasema kina wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokuwepo kwa mgombea wake kwenye orodha iliyochapishwa na Ceni. © REUTERS/Kenny Katombe
Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi inatarajia kutangaza orodha ya wagombea ambao wanatimiza vigezo na masharti ya kuwania katika Uchaguzi Mkuu nchini DRC, kabla ya Mahakama ya Katiba kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea Septemba 19.

Zoezi la kuchunguza vigezo hivyo liliendelea hadi usiku wa manane Alhamisi wiki hii. Kwa upande wa CENI, wanasema itakua suala la kuchagua wale ambao, kati ya wagombea wa uchaguzi wa urais ule wa wabunge, wanaotimiza vigezo na masharti ya kuwania katika uchaguzi huo kama inavyoelezwa katika sheria ya uchaguzi.

Watu ishirini na tano ndio waliwasilisha fomu zao za kuwania katika uchaguzi wa rais na watu elfu kumi na tano na mia sita na sabini katika uchaguz wa wabunge wa kitaifa.

Wengi wamekua wakijiuliza kuhusu vigezo hivyo na masharti, wakibaini kwamba huenda ni katika hali ya kuwatenga baadhi ya wanasiasa wakuu wa upinzani wenye ushawishi mkubwa nchini DRC. Chama cha upinzani cha MLC, kimekua kikitoa malalamiko yake dhidi ya uwezekano wa kutoidhinishwa kwa kiongozi wake Jean Pierre Bemba, mgombea wa urais.

Pia kuna orodha ya watu wanaoshukiwa kuwa ni raia wa DRC ambao wana uraia wa kigeni, ambayo imewasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi, CENI, kwa ombi la Waziri wa Sheria. Kuna uwezekano watu hao wakataliwe kuwania katika uchaguzi Mkuu nchini DRC.

Wakati huo huo shirika linalotetea haki kwa wote, ACAJ, limeomba Tume ya Uchaguzi kutochukua nafasi ya mahakama, kuheshimu sheria inayoihusu kama chombo kinachosaidia kuimarika kwa demokrasia na kuachia Mahakama ya Katiba kufanya kazi yake.