AFRIKA KUSINI-USALAMA

Afrika Kusini yakumbwa tena na ghasia za ubaguzi

Wanawake wawili wakiondoka katika duka linalomilikiwa na raia wa kigeni huko Soweto na kikapu kilichojaa bidhaa Januari 22, 2015.
Wanawake wawili wakiondoka katika duka linalomilikiwa na raia wa kigeni huko Soweto na kikapu kilichojaa bidhaa Januari 22, 2015. REUTERS/Siphiwe Sibeko

Ghasia za ubaguzi zimeibuka tena nchini Afrika Kusini, hasa katika maeneo mengi ya Soweto. Watu wawili waliuawa katika mapigano yaliyotokea kati ya wenyeji na wageni katika mji wa Soweto, kwa mujibu wa polisi.

Matangazo ya kibiashara

Shughuli katika maeneo mengi ya Soweto zilizorosta, huku maduka yanayomilikiwa na wageni yakiporwa bidhaa kufuatia ghasia hizo.

Idadi ya maduka haya yanayomilikiwa na wageni yamejengwa katika maeneo ya karibu na makazi na yamekuwa yakimilikiwa raia pia kutoka nchi nyingine kama vile Ethiopia, Zimbabwe na Pakistan.

Hali hiyo pia imewafanya wamiliki wengi wa maduka kufungasha bidhaa zao na kuondoka mjini humo wakihofia vurugu zaidi.

Kwa mujibu wa polisi ghasia hizo zilianzia katika duka moja, baada ya wakazi wa eneo hilo kumtuhumu mmiliki wa duka mwenye asili ya Somalia kumshambulia kwa risasi na kumuua kijana mdogo aliyedai kuwa alikuwa akijaribu kuvunja duka lake.

Wakazi hao pia wanawalaumu wamiliki wa maduka, ambao wengi ni wageni, kuuza vyakula vilivyopitwa na wakati.

Kwa mujibu wa masahahidi, kuna ujumbe wa WhatsApp ambao umekuwa ukizunguuka nchini Afrika kusini ukimuonya yeyote yule, aliyepangisha vyumba kwa raia wa kigeni hasa Wasomali, kuwafukuza haraka kabla ya tarehe 8 Septemba mwaka huu, la sivyo nyumba zote na maduka yatachomwa moto.