DRC: Mahakama ya Katiba yatathmini malalamiko ya wagombea waliokataliwa na CENI

Tangu Jumatano, Agosti 29, Mahakama ya Katiba ya DRC inatathmini malalamiko yaliyowasiliswa na wagombea sita wa urais ambao fomu zao zilibatilishwa na Tume ya Uchaguzi ( CENI). Utaratibu kwenye mahakama utadumu siku saba, kwa mujibu wa chanzo cha mahakama.

Kikao cha Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Oktoba 2015. (Picha ya kumbukumbu).
Kikao cha Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Oktoba 2015. (Picha ya kumbukumbu). Chancelfun/wikimedia commons
Matangazo ya kibiashara

Msemaji, pia katibu wa vikao vya Mahakama ya Katiba, Kahozi Lumwenga, amethibitisha kuwepo kwa malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani na wagombea wote wa urais waliokataliwa na CENI. "Ni wagombea sita ambao maombi yao yalibatilishwa. Hawa ndio ambao wamewasilisha malalamiko yao mbele ya Mahakama ya Katiba, " amesema Bw Lumwenga.

Utaratibu wa Mahakama ulianza Jumatano, Agosti 29. Kwa mujibu wa sheria, mahakama ina siku saba ili kutoa uamuzi wake kuhusu uchaguzi wa urais ambao ulipangwa kufanyika Desemba 23.

"Katika hatua ya kwanza, kutakuwa na majadiliano yatakayofanyika, ambapo wagombea au wanasheria wao watasikilizwa na Mahakama itachunguza na kujadili kwa undani malalamiko yao na kusikiliza upande wa Tume ya Uchaguzi. Majaji watakutana kwa katika kikao maalumu. Siku ya saba, mahakama itatoa uamuzi wake, " ameongeza Bw Lumwenga.

Wakati wa kesi hiyo, CENI pia itaalikwa kuelezea sababu za zilizopelekea kuchukua hatu ya kuwaondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais wagombea hao sita waliowasilisha malalamiko yao mbele ya Mahakama ya Katiba.

Je! Tunaweza kuwa na imani na majaji wa mahakama hii? "Sheria zipo. Wakati sheria inazungumzia kitu fulani, nadhani tunapaswa kuamini Mahakama hii, ambayo ni mama wa Katiba, "amejibu Kahozi Lumwenga.

Kwa upande wa upinzani, wanasema hii ni fursa ya Mahakama ya Katiba kuonyesha uhuru wake.