SENEGAL-SALL-SIASA-HAKI

Meya wa Dakar athibitishiwa kifungo cha miaka mitano Senegal

Mahakama ya Rufaa imethibitisha kifungo cha miaka mitano kwa aliyekuwa meya wa Dakar Khalifah Sall. Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa uliyotolea leo Alhamisi mjini Dakar ni pigo kubwa kwa muhusika ambaye unaweza kumuondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais nchini Senegal.

Khalifa Sall akiwasalimu wafuasi wake siku ya kwanza ya kesi yake kataika Mahakama ya Rufaa, Julai 9.
Khalifa Sall akiwasalimu wafuasi wake siku ya kwanza ya kesi yake kataika Mahakama ya Rufaa, Julai 9. RFI/Guillaume Thibault
Matangazo ya kibiashara

Ni pigo kubwa bila shaka lakini hukumu hii ilikua inatarajiwa, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vilivyo karibu na meya wa Dakar. Hata hivyo uamuzi huo ulitangazwa wakati Khalifa Sall hakuwepo mahakamani.

Baadhi ya wanasheria wake waliwasili mahakamani lakini walikua hawakuvaa nguo zao za kazi kama ishara ya kupinga utaratibu unaotumiwa kwa kuendesha kesi hiyo. Wamebaini kwamba kesi hii katika Mahakama ya Rufaa ilikua kama kiini macho tu kwa lengo la kumtenga Khalifa Sall kuwania katika uchaguzi wa urais.

Pia Mahakama ya Rufaa imemtaka Khalifa Sall na watuhumiwa wenzake wawili kuilipa serikali fedha za nchi hiyo, CFA, bilioni 1,230 kama fidia.

Hata hivyo Khalifa Salla bado ana njia ya mwisho ya kukata rufaa. Kwa mujibu wa wadadisi Khalifa Sall sasa anataka kuokoa muda kabla ya uamuzi wa mwisho wa mahakama, ambao unaweza kumzuia kuwania katika uchaguzi wa urais. Julai 26 alitangaza kwamba atawania katika uchaguzi ujao wa urais uliopangwa kufanyika mnamo mwezi Februari 2019.