AFRIKA-CHINA-UCHUMI

Viongozi wa Afrika wamiminika China, kuhudhuria kongamano la kiuchumi la China-Afrika

Rasi wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe Janet Museveni wakiwasili nchini China kuhudhuria Mkutano wa Kiuchumi baina ya China na Afrika
Rasi wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe Janet Museveni wakiwasili nchini China kuhudhuria Mkutano wa Kiuchumi baina ya China na Afrika Twitter/Yoweri Museveni

Idadi Kubwa ya viongozi wa Afrika wapo nchini China, kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa ushirikiano baina ya Afrika na China.

Matangazo ya kibiashara

Huu ni mkutano wa tatu tangu kuasisiwa kwa ushirikiano baina ya China na Afrika, mkutano wa kwanza ulifanyika mwaka 2006 Mjini Beijing na wa pili ulifanyika mwaka 2015 nchini Afrika Kusini.

Mkutano huu unawakutanisha viongozi wa Afrika na Uchina, ukilenga kujadili njia za kukuza uhusiano katika nyanja ya kiuchumi na kidemokrasia.

Baadhi ya viongozi waliowasili nchini China ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi,Edgar Lungu wa Zambia, Adama Barrow wa Gambia na Peter Mutharika wa Malawi.

Mkutano huo pia unahudhuriwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Gutterres.

Li Dan, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika katika Chuo Kikuu cha Mambo ya nje ya Uchina amesema Jukwaa hilo kwa kipindi cha miaka 18 limesaidia kukuza ushirikiano wa nchi za ukanda wa kusini (South-South Cooperation).

China imekuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika, ikijihusisha kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli katika mataifa ya Kenya na Ethiopia. Hata hivyo wakosoaji wa uwekezaji unaofanywa na China barani Afrika wanasema unoangeza madeni kwa mataifa ya Afrika.