MAURITIUS-UINGEREZA-ICJ-HAKI

ICJ kuchunguza mgogoro kati ya London na Port Louis kwenye visiwa vya Chagos

Kesi ikisikilizwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kesi ikisikilizwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ). UN Photo ICJ-CIJ/Frank Van Book (United Nations)

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) leo Jumatatu inachunguza mgogoro kati ya Uingereza na Mauritius kuhusu Visiwa vya Chagos ambapo kila upande unadai kuwa ni eneo lake.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa kutoka Uingereza, Visiwa vya Chagos vinapatikana kwenye rasi ya Uingereza katika Bahari ya Hindi ambako kumejengwa kambi kubwa ya jeshi la Marekani, eneo linalodaiwa na Mauritius kuwa ni eneo lake.

Wawakilishi wa Port Louis wanatarajia kufungua mashtaka mbele ya mahakama ya Hague kuhusu mgogoro unaosababishwa na uamuzi wa wakoloni wa Uingereza wa kutenganisha rasi hii kutoka Mauritius mnamo mwaka1965 na kupajenga kambi ya pamoja ya jeshi la Uingereza na Marekani kwenye kisiwa kikuu cha Diego Garcia.

Mnamo mwezi Juni 2017, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio lililotolewa na Mauritius na kuungwa mkono na nchi za Afrika ikiomba ICJ kutoa maoni yake ya ushauri kkuhusu mgogoro kongwe, wa tangu miaka hamsini iliyopita.

Majaji15 wa mahakama wanatarajia kusikia hoja juu ya "matokeo ya kisheria ya kutenganisha rasi ya Chagos kutoka Mauritius", zoezi lililofanyika miaka mitatu kabla ya Port Louis kupata uhuru wake mwaka 1968.

Umoja wa Afrika na nchi 22, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani, Ujerumani na nchi kadhaa za Asia na nchi kadhaa za Kusini mwa Amerika, wanatarajiwa kushiriki katika kesi hii itakayodumu siku nne mbele ya ICJ .

Kisha, taasisi kuu ya mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, inayohusika na kuchunguza migogoro ya kisheria kati ya Mataifa, itatoa "maoni ya ushauri".