LIBYA-USALAMA

Mamia ya wafungwa watoroka karibu na mji wa Tripoli

Moshi mkubwa ukifunba eneo jirani ya Tripoli ambako kunashuhudiwa mapigano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo Agosti 28, 2018.
Moshi mkubwa ukifunba eneo jirani ya Tripoli ambako kunashuhudiwa mapigano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo Agosti 28, 2018. REUTERS/Hani Amara

Wafungwa zaidi ya 400 wametoroka baada kuzuka ghasia katika jela iliyoko katika kitongoji kimoja kusini mwa Libya, mji mkuu Tripoli, ambako mapigano yanaendelea kwa wiki moja sasa, polisi imeangaza katika taarifa yake.

Matangazo ya kibiashara

"Wafungwa walibomoa milango na kutoka nje" baada ya "kuzuka ghasia" kutokana na mapigano kati ya wanamgambo hasimu karibu na gereza la Aine Zara, polisi imesema bila hata hivyo kubainisha kama wafungwa waliotoroka walikua wamehukumiwa kwa makosa madodo madogo au la.

Polisi magereza hawakuingilia kati ili kuachia wafungwa hao "kuokoa maisha" yao, polisi imeongeza.

Akihojiwa na shirika la Habari la AFP, msemaji wa mahakama, amesema hawezi kutoa maelezo zaidi.

Wengi wa wafungwa katika jela la Aine Zara walihukumiwa kwa makosa madogo madogo na wengine ni wafuasi wa zamani wa serikali ya zamani ya Muammar Gaddafi ambao walihukumiwa kwa mauaji ikiwa ni pamoja na uasi wa mwaka 2011.

Makundi hasimu ya wanamgambo yanapambana tangu Jumatatu wiki iliyopita kwa silaha za kivita katika vijiji vya kusini mwa mji mkuu wa Libya. Mapigano hayo yameua kwa uchache watu arobaini na zaidi ya 100 wamejeruhiwa kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya.