UN : Makundi hasimu yamekubali kusitisha mapigano karibu na Tripoli

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo katika mji wa Sabratha, mji ulio kilomita 70 magharibi mwa Tripoli.
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo katika mji wa Sabratha, mji ulio kilomita 70 magharibi mwa Tripoli. MAHMUD TURKIA / AFP

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umetangaza kwamba makundi ya waasi yamefikia mkataba wa kusitisha mapigano karibu na mji mkuu wa Libya Tripoli. Mapigano ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya hamsini tangu Agosti 27.

Matangazo ya kibiashara

"Chini ya mwamvuli wa Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya Ghassan Salamé, mkataba wa kusitisha mapigano uliafikiwa na kutiliwa saini leo (Jumanne) ili kukomesha uhasama, kulinda raia na kulinda mali ya serikali na ya raia".

Kazi ya UNSMIL itakua ngumu kutokana na idadi ya wanaohusika katika mapigano ambayo yameua watu zaidi ya 50 na 138 kujeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti rasmi ya mwisho iliyotolewa siku ya Jumatatu usiku.

Mapigano hayo yamesababisha familia 1,825 kuyahama makazi yao na kukimbilia miji jirani au maeneo mengine salama katika mji mkuu wa Libyan, kulingana na Wizara yenye dhamana ya wakimbizi wa ndani.

Asilimia moja ya familia zilizokwama katika mapigano zimekataa kuondoka katika nyumba zao kwa hofu ya kuibiwa mali zao.

Familia nyingi zilizokwama katika maeneo hayo ya mapigano zinahitaji haraka chakula na maji, kulingana na ripoti ya wizara yenye dhamana ya wakimbizi wa ndani ambayo inasema kumekuwepo na mashambulizi ya dhidi ya maafisa wa idara ya dharura na "wizi" wa magari ya wagonjwa, bila kubainisha wahalifu wa mashambulizi haya.

Ripoti hiyo inatarajia wimbi jipya la wakimbizi ikiwa mapigano yatakaribia katikati mwa mji mkuu.

Mapigano hayo ni kati ya makundi kutoka Tarhouna na Misrata, magharibi mwa nchi dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha kutoka Tripoli yanayodhaminiwa na serikali.