GHANA-UN-JAMII

Mwili wa Kofi Annan wawasili Ghana na kuzikwa Alhamisi

Mtu huyu akiwa mbele ya picha ya aliye kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani, Agosti 28, 2018.
Mtu huyu akiwa mbele ya picha ya aliye kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani, Agosti 28, 2018. © REUTERS

Mwili wa Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan umewasili nchini Ghana, ambako alizaliwa. Koffi Annan alifariki mwezi uliopita. Anatarajiwa kuzikwa kitaifa siku ya Alhamisi.

Matangazo ya kibiashara

Mke wake, Nane Maria Annan, watoto wake na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wasindikiza jeneza kutoka Geneva, nchini Uwisi, jeneza ambalo lilikuwa limefunikwa bendera ya bluu ya Umoja wa Mataifa.

Kofi Annan, Mwanadiplomasia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel - kiongozi wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika- alifariki dunia Agosti 18 akiwa na umri wa miaka 80.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo alikuwapo kwenye sherehe ya kuwasili kwa mwili wa Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja w Mataifa. Viongozi wa jadi, viongozi maarufu wa kidini, viongozi wakuu wa kijeshi na wanasiasa mbalimbali nchini Ghana walihudhuria sherehe hiyo.

Jeneza lilipokelewa na askari sita wa Ghana. Bendera ya Umoja wa Mataifa iliyokua imewekwa kwenye jeneza ilibadilishwa na bendera ya Ghana - nyekundu, njano na kijani.

Watu wataruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho kwa Kofi Annan tangu leo Jumanne.

Viongozi wengi kutoka duniani kote wanatarajiwa siku ya Alhamisi kwa mazishi ya kitaifa.

Kofi Annan, ambaye alikua akiishi nchini Uswisi, atazikwa katika kaburi jipya la kijeshi la Accra, mji mkuu wa nchi ndogo ya Magharibi mwa Afrika, "mahali panapofaa zaidi kwa msitiri Kofi Annan," alitangaza mwishoni mwa mwezi Agosti Rais Nana Akufo-Addo, baada ya kukutana na familia ya marehemu.

"Itakuwa tukio kubwa kwa nchi yetu," aliongeza.

Baada ya tangazo la kifo cha Kofi Annan, serikali ya Ghana ilitangaza wiki moja ya maombolezo ya kitaifa, huku bendera zikipandishwa nusu mlingoti.