LIBYA-UN-USALAMA-SIASA

Umoja wa Mataifa waongezea ujumbe wake muda wa mwaka mmoja Libya

Wahusika wakuu wa katika mgogoro wa Libya na wawakilishi wa kigeni walikutana katika ikulu ya Elysée Mei 29, 2018.
Wahusika wakuu wa katika mgogoro wa Libya na wawakilishi wa kigeni walikutana katika ikulu ya Elysée Mei 29, 2018. Etienne Laurent/Pool via Reuters

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limepitisha azimio linaloongezea ujumbe wake nchini Libya muda wa mwaka mmoja, bila hata hivyo kuweka tarehe ya uchaguzi. Hivi karibuni Ufaransa ulipendekeza Uchaguzi Mkuu nchini Libya kufanyika tarehe 10 Desemba 2018.

Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita, wakati wa mkutano kuhusu Libya, Ufaransa ilipendekeza kuwepo na "umuhimu wa kuendeleza mchakato wa kidemokrasia nchini Libya" na "kuandaa uchaguzi kulingana na kalenda iliyokubaliwa na wadau muhimu katika siasa ya Libya mjini Paris mnamo Mei 29 ".

Wakati wa mkutano huo, wadau katika mazungumzo hayo walikubaliana uchaguzi kufanyika tarehe 10 Desemba 2018. Makubaliano hayo yalifikiwa chini ya shinikizo la Ufaransa ambayo inasema kwamba "adui wa Libya na Walibya ni hali ya kisiasa inayoendelea nchini humo".

Katika nakala yake, iliyoandikwa na Uingereza, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeitaka Libya kuhakikisha "uchaguzi unafanyika haraka iwezekanavyo".

Azimio hilo pia linasisitiza haja ya kufanyika kwa "uchaguzi wa kuaminika" na kuomba nchi wanachama "kusitisha msaada wowote na mawasiliano na taasisi zinazoendesha sambamba majukumu ya nchi".

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani na Italia, hawaungi mkono pendekezo la Ufaransa na kusisitiza wajibu wa kufikia kuunganishwa kwa taasisi za Libya kabla ya kwenda kwenye hatua ya uchaguzi.

Libya inaongozwa na serikali ya umoja wa serikali (GNA) inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa. Lakini kiongozi wake Fayez al-Sarraj, ambaye makao yake makuu ni mjini Tripoli, hana mamlaka katika eneo la mashariki ya nchi, eno linalodhibitiwa na Marshal Khalifa Haftar.

Miaka saba baada ya kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi, makundi mengi ya kijihadi na makundi ya wanamgambo wenye silaha wanaendelea kujidhatiti na kuhatarisha usalama wa taifa.