DRC-ICC-SIASA

Kesi ya Jean-Pierre Bemba: DRC yatishia kujitoa ICC

Kiongozi wa upinzani DRC Jean-Pierre Bemba wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Kinshasa, Agosti 3, 2018.
Kiongozi wa upinzani DRC Jean-Pierre Bemba wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Kinshasa, Agosti 3, 2018. REUTERS/Kenny Katombe

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetishia kujitoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Kauli hiyo ya serikali ya DRC inakuja wakati Mahakama ya Kimataifa ya ICC inatarajia kutoa uamuzi wake dhidi ya Jean-Pierre Bemba kuhusu kuhonga mashahidi Jumatatu wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni taarifa nzito ambayo wizara ya mambo ya nje ya DRc imetoa. Wizara hiyo inazungumzia shinikizo kutoka kwa baadhi ya serikali kwa majaji wa ICC. "Kuna baadhi ya nchi ambazo zimekua zikitoa ushawishi kwa Mahakama hii ya Kimataifa kwa malengo ambayo hayaeleweki na hivyo kuhatarisha kwa kiasi kikubwa uaminifu kwa chombo hiki," wizara ya mambo ya nje imeleza katika taarifa hiyo.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inatarajia kutoa uamuzi wake dhidi ya Jean-Pierre Bemba na baadhi ya washtakiwa wengine. Majaji wa ICC wananatarajia kutoa hukumu yake Jumatatu hii, Septemba 17, baada ya kupatikana na hatia ya kuhonga mashahidi.

Mahakama ya Katiba ilithibitisha uamuzi wa CENI wa kumzuia Jean- Pierre Bemba kuwania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23 na kusema kuwa hana sifa ya kuwania katika uchaguzi huo kufuatia hukumu aliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kosa la kuhonga mashahidi.

Hivi karibuni chama cha kiongozi wa zamani wa kivita Jean-Pierre Bemba kilitoa wito kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu "kuweka mambo sawa" kuhusu sheria iliyomhukumu Bemba kwa kosa la kuhonga mashahidi.

Jean-Pierre Bemba anatajwa kama mpinzani mkuu anayesumbua utawala wa Joseph Kabila na chama chake cha PPRD katika uchaguzi ujao.

Hivi karibuni Bemba aliachiliwa katika kesi dhidi ya uhalifu wa kivita na mahakama baada ya kutumikia kifungo cha miaka kumi jela.

Mwezi uliopita alirejea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kupokelewa kwa mapokezi makubwa kutoka kwa wafuasi wake.