DRC-UN-HAKI

UN: Visa vya uvunjifu wa haki za binadamu vimeongezeka DRC

Polisi ikikabiliana na waandamanaji karibu na Kanisa kuu la Notre Dame Kinshasa, DRC tarehe 25 Februari 2018.
Polisi ikikabiliana na waandamanaji karibu na Kanisa kuu la Notre Dame Kinshasa, DRC tarehe 25 Februari 2018. REUTERS/Goran Tomasevic

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) imesema, vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vimeongezeka ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa rais na ule wa wabunge wa kitaifa na wa mikoa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa ripoti iliotolewa hivi karibuni na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (Monusco) kwa mwezi wa nane, vitendo 620 vimeorodheshwa, sawa na vitendo vya kuwatisha watu, kuwakamata kinyume cha sheria, mauaji wakati vyombo vya sheria vikituhumiwa kuhusika na asilimia 66 ya uvunjifu wa vitendo hivyo.

Idadi hii imeongezeka mara mbili zaidi ikilinganishwa na mwezi Julai, sababu hasa inaelezwa kuwa ni kutokana na kupanda kwa joto la kisiasa kuelekea katika uchaguzi mkuu ambapo kumeshuhudiwa vitendo vya vitisho, kamatakamata, kusambaratisha maandamano. Polisi ndio inayonyooshewa kidole, huku waathirika wakuu wakiwa ni wafuasi wa vyama vya siasa.

Umoja wa Mataifa umesema tangu kuteuliwa kwa mrithi wa rais Joseph kabila mwanzoni mwa mwezi Agosti, matukio ya vitisho yameongezeka, zaidi ya watu 40 wamejikuta usalama wao ukiwa hatarini kutokana na vitisho. Wanaharakati wa haki za binadamu wapatao 29, mashahidi 10 wamehusishwa katika matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu akiwemo mwandishi wa habari.

Mbali na hayo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu imesema inatiwa wasiwasi na idadi ya watu wanaopoteza maisha wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola au makundi ya waasi ambapo kwa siku mtu mmoja hupoteza maisha akiwa mikononi mwa polisi, na wawili hupoteza maisha wakiwa mikononi mwa wapiganaji waasi. Katika eneo la mashariki, makundi ya FDLR na Mai-Mai Mazembe yametajwa kuwa makundi husika, huku eneo la Kivu Kaskazini kundi la FRPI katika jimbo la Ituri pamoja na kundi la Raia Mutomboki katika mkoa wa Kivu Kusini.