CAMEROON-SIASA

Kampeni za uchaguzi zaanza rasmi Cameroon

Rais aw cameroon Paul Biya.
Rais aw cameroon Paul Biya. AFP

Kampeni za kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa Octobea 7 nchini Cameroon, zimefunguliwa rasmi huku kwa mara ya kwanza wagombea karibu wote wakitumia mitandao ya kijamii kujinadi.

Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni Rais wa Cameroon Paul Biya, ambae kwa sasa ana umri wa miaka 85 alitangaza kuwa atawania kiti cha urais katika uchaguzi huo.

Taarifa hiyo, rais Biya aliitoa kupitia ukurasa wake Twitter.

Hata hivyo ni wagombea wanne kati ya 9 wanaopewa nafasi kwenye uchaguzi unaokuja, akiwemo rais wa sasa Paul Biya ambaye alizindua kampeni zake jijini Yaounde, huku wapinzani wake wakienda kwenye miji ya Douala na Bamenda ambako wananchi wengie wanazungumza kingereza.

Iwapo Paul Biya atachaguliwa atakuwa anaingoza Cameroon katika muhula wake wa 7.

Serikali ya Cameroon tayari imeahidi kwamba, itafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu na katika maeneo yote ya nchi, licha ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kushuhudia machafuuko katika maeneo ambayo wakazi wake wanazungumza Kiingereza.

Paul Atanga Nji, Waziri wa Utawala wa Cameroon amesema kuwa, uchaguzi wa urais wa mwezi ujao wa Oktoba 7 utafanyika katika mazingira mazuri na amani nchini kote na kwamba, serikali ya nchi hiyo imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kwamba, zoezi hilo la uchaguzi linafana.

Aidha Rais Paul Biya wa nchi hiyo amezitaka mamlaka husika kufanya kila ziwezalo kuhakikisha kwamba, uchaguzi ujao unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.

Maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza nchini Cameroon yalitumbukia katika mgogoro wa kijamii na kisiasa sambamba na kuongezeka maandamano tangu mwezi Novemba mwaka 2016 baada ya wakazi wa maeneo hayo kudhihirisha azma yao ya kutaka kujitenga.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakivitaka vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kutotumia mbinu za ukatili kuzima malalamiko na maandamano ya wananchi wanaotaka majimbo yao yajitenge na serikali kuu ya Yaounde.