GHANA-MAREKANI-MELANIA-USHIRIKIANO

Melania Trump awasili Ghana

Mkewe rais wa Marekani Donald Trump, Melania Trump amewasili Jumanne wiki hii nchini Ghana, hatua ya kwanza katika ziara yake ya wiki moja barani Afrika.

Mkewe rais wa Marekani Donald Trump, Melania Trump na Mkew rais wa Ghana Rebecca Akufo-Addo kwenye uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kotoka  Accra, Ghana Oktoba 2, 2018.
Mkewe rais wa Marekani Donald Trump, Melania Trump na Mkew rais wa Ghana Rebecca Akufo-Addo kwenye uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kotoka Accra, Ghana Oktoba 2, 2018. © AP
Matangazo ya kibiashara

Trump aliwasili mji mkuu wa Ghana, Accra, mchana. Umati wa watoto walio kuwa wamevalia sare ya njano na kahawia, rangi ya bendera ya Ghana na makundi ya wanamuziki wa jadi walikuja kumlaki Melani trump kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kokota.

Melania Trump alipokelewa na mkewe rais wa Ghana Rebecca Akufo-Addo.

Hii ni ziara ya kwanza ya Melania Trump, mwana mitindo wa zamani, Mmarekani mwenye asili ya Slovenia kuzuru bara la Afrika.

Ziara ya Melania barani Afrika inalenga kuhamasisha ulinzi wa haki za watoto pamoja na mazingira bora ya utoaji elimu kwenye mataifa atakayotembelea.

Kulingana na maneno ya msemaji wake Stephanie Grisham, ziara ya mke wa tatu wa Rais wa Marekani imetokana na kazi ambazo zinafanywa na shirika la misaada la Marekani USAID kwa nchi za Afrika, ambapo amesema maeneo ambayo shirika hilo limekuwa likifanyia kazi yamekuwa ni sehemu ya maisha yake.

Melania amesema anatarajia ziara yake kwenye mataifa hayo kuwa yenye tija hasa wakati huu ambapo mtoto wa kiafrika ameendelea kukabiliwa na changamoto za kielimu, matumizi ya dawa za kulevya, unyanyasaji, usalama katika matumizi ya mtandao, umasikini na magonjwa, akisema katika karne hii watoto hawapaswi kuwa katika mazingira haya, amesema Stephanie Grisham.

Melania Trump katika ziara yake hiyo barani Afrika baada ya Ghana atazuru Malawi Kenya, Misri.