COTE D'IVOIRE-ICC-HAKI

Ombi la Gbagbo la kuachiliwa huru ICC laingiliwa na upinzani

Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, Januari 28, 2016, wakati wa kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Hague (Uholanzi).
Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, Januari 28, 2016, wakati wa kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Hague (Uholanzi). ICC-CPI

Wakati kesi ya Laurent Gbagbo na waziri wake wa zamani Charles Blé Goudé ikianza mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Jumatatu Oktoba 1, upande wa mashitaka umeendelea kuonyesha kuwa wawili hao wanakabiliwa na uhalifu dhidi ya binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Upande wa mashitaka umebaini kwamba Laurent Gbagbo na Charles Ble Goude walihusika katika mauaji wakati wa machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2010.

Upande wa mashitaka umesema una ushahidi tosha dhidi ya watuhumiwa hao.

Hata hivyo wanasheria wa upande wa utetezi wamefutilia mbali ushahidi huo wa upande wa mashitaka na kusema kuwa wiki hii wataomba wateja wao waachiliwe huru, kwani hawana hatia yoyote. Akijibu kuhusu hoja ya upande wa utetezi, Eric MacDonald, msaidizi wa mwendesha mashitaka ambaye anashikilia kesi hii kwa zaidi ya miaka miwili sasa, amefutilia mbali hoja zao.

Bw MacDonald amesema watuhumiwa walihusika katika machafuko yaliyoikumba Cote d'Ivoir wakati wa machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi, huku akieleza tukio baada kwa tukio.

"Watu wengi waliuawa wakati wa maandamano kwenye makao makuu ya shirika la utangazaji la RTI Desemba 16, 2010 kwa amri ya Laurent Gbagbo, " amesema Bw MacDonald, huku akionyesha tukio jingine la mashambulizi ya anga katika kata ya Abobo mnamo Machi 2011 na mauaji ya raia wa kawaida katika mji wa Yopougon mwezi mmoja baadaye. Kwa mujibu wa Eric MacDonald "hakuna shaka ushahidi tosha dhidi ya kambi ya Gbagbo upo.

Charles Blé Goudé et Laurent Gbagbo, en octobre 2010 pendant la campagne présidentielle, avant la crise post-électorale.
Charles Blé Goudé et Laurent Gbagbo, en octobre 2010 pendant la campagne présidentielle, avant la crise post-électorale. AFP PHOTO/ SIA KAMBOU

Gbagbo, mwenye umri wa miaka 73, ndiye rais wa kwanza kuwasilishwa katika Mahakama ya ICC ya Hague, ambako kesi yake imekuwa ikisikilizwa tangu mwaka 2016.

Rais huyo wa zamani, anakabiliwa na mashtaka manne, yote ya ukiukwaji wa haki dhidi ya binadamu, kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea baada ya Uchaguzi tata wa urais mwaka 2010 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 3000.

Mawakili wake wanasema wana uhakika kuwa mteja wao ataachiliwa huru, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kubaini iwapo Ggagbo alihusika na makosa hayo.