COMORO-SIASA-USALAMA

Jeshi laingilia kati kwa kuondoa vizuizi katika kisiwa cha Anjouan

Kisiwa cha Anjouan, Comoro.
Kisiwa cha Anjouan, Comoro. CC BY-SA 3.0/Haryamouji/Wikimedia Commons

Vikosi vya usalama na ulinzi vya Comoro vimeingilia kati kwa kufyatua risasi hewani katika mji mkuu wa kisiwa cha Anjouan, Mutsamudu, ili kuondoa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa kwenye barabara kadhaa za mji huo, kwa mujibu wa mashahidi.

Matangazo ya kibiashara

"Hali hiyo ilianza karibu mapema asubuhi na ilidumu saa tatu, tulisikia milio mingi ya risasi, milio mingi kabisa ...", amesema mkaazi wa mji huyo ambaye hakutaja jina akihojiwa na shirika la Habari la AFP mjini Moroni.

Akihojiwa na shirika la Habari la AFP, Gavana wa Kisiwa hicho, Abdou Salami Abdou, kutoka chama cha upinzani Juwa, amethibitisha tukio hilo. "Ndio,hali hiyo ilianza tangu mapema asubuhi , milio ya risasi inasikika sehemu zote," amesema kwenye simu.

Hali ya kisiasa inakumbwa na sintofahamu kwa miezi kadhaa nchini Comoro, ambapo Rais Azali Assoumani hivi karibuni alichukuwa hatua ya kukamatwa wanasiasa wa upinzani.

Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliokamatwa ni pamoja na rais wa zamani wa rasi hiyo Abdallah Sambi, ambaye anashtumiwa kuhusika katika madai ya rushwa. Bw Sambi ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Juwa, ni kutoka mji wa Anjouan.

Vizuizi hivyo viliwekwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo (Habomo, Fortaleza, Mroni, eneo la sokoni, nk ...) na barabara nyingi za mji mkuu zilifungwa, kwa mujibu wa wakazi wa mji huo.

Joto la kisiasa limeendelea kupanda nchini Comoro baada ya mamlaka ya Rais Azali Assoumani kupewa uwezo zaidi kupitia kura ya maoni, ambapo kura ya Ndiyo ilishinda kwa 92,74% ya kura, huku upinzani ukisusia.