DRC-EBOLA-AFYA

Ebola yaua watu 170 mashariki mwa DRC

Kitengo kinachohusika na kuwaondoa wagonjwa wa Ebola katika makazi ya watu, DRC wakati wa mlipuko wa virusi vya Ebola mwaka 2009.
Kitengo kinachohusika na kuwaondoa wagonjwa wa Ebola katika makazi ya watu, DRC wakati wa mlipuko wa virusi vya Ebola mwaka 2009. Luis Encinas/MSF

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC, imefikia 170. Mapema wiki iliyopita Umoja wa Ulaya ulisema unatoa Euro Milioni 7.2 kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu hizi zimetolewa na Wizara ya afya ambayo imesema, idadi hiyo imepanda baada ya kuripotiwa kwa visa 267 vya maambukizi katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Hata hivyo kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya tarehe 26 Oktoba 2018, hadi siku ya Ijumaa wiki iliyopita idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia ugonjwa wa Ebola ilikuwa imefikia 168.

Mashirika ya kiraia yanasema yanaendelea na harakati za kutoa elimu kwa uma Wilayani Beni, licha ya kukabilianana changamoto mbalimbali.

Wiki tatu zilizopita, WHO ilionya kuwa, kuna hatari ya maambukizi hayo kuendelea kuenea iwapo visa vya maambukizi havitapungua.

Mkoa wa Kivu Kaskazini ndio unaathiriwa hasa Wilaya ya Beni, na idadi ya watu walipoteza maisha inaendelea kuongezeka kila kukicha.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani linasema maambukizi hayo hayajafikia kiwango cha kutisha na kuathiri maeneo mengine duniani.

Takwimu kutokana na mlipuko uliopo sasa wa Ebola nchini DRC, unaonyesha kwamba kati ya watu 10 walioambukizwa Ebola 6 hufariki dunia.