DRC-SIASA-USALAMA

Tume Huru ya Uchaguzi DRC yazindua radio yake

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) imezindua radio yake na lengo lake ni kutangaza kuhusu mchakato wa uchaguzi na itasikika nchini kote, amesema Mwenyekiti wa CENi Corneille Nangaa.

Mwenyekiti wa CENI DRC, Corneille Nangaa, Novemba 5, 2017 Kinshasa
Mwenyekiti wa CENI DRC, Corneille Nangaa, Novemba 5, 2017 Kinshasa © JOHN WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya tume hiyo kuonesha vifaa, magari na ndege ilizokabidhiwa na jeshi ambavyo vitatumika katika uchaguzi wa Desemba 23. Katika hatua nyingine, pamema wiki hii Ceni ilipokea mashine za kupigia, ambazo zimezua utata nchini DRC na kusababisha mvutano wa kisiasa katika nchi hiyo tajari Afrika ya Kati na ambayo inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Corneille Nangaa amesema radio hiyo haitoegemea upande wowote na itahudumia wananchi wote na wanasiasa kutoka vyama mbalimbali.

"Radio Ceni inapaswa kuwa radio isiyoegemea upande wowote. Hii sio radio ambapo wanasiasa watapewa nafasi ya kutoa maoni yao ya kisiasa kwa mchakato wa uchaguzi unaoendelea. Radio Ceni itatoa habari zinazohusu tu uchaguzi na imeanzishwa ili kuwahabarisha wapiga kura na vyama vyote kuhusu mchakato wa uchaguzi na matokeo ya uchaguzi kutoka maeneo mablimbali, "amesema Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwa upande wao, wanasiasa wa upinzani, ambao wamekuwa wakishtumu vyombo vya habari vya serikali kuwa vibaraka wa viongozi waliopo madarakani, wana hofu kwamba radio Ceni itatumiwa na haitotoa habari zilizosahihi.

Kwa upande mwengine, Ndombi Tito, Mwenyekiti wa Mamlaka inayochunguza Vyombo vya Habari na Mawasiliano (CSAC), ana matumaini kwamba radio hii mpya itakuwa mfano mzuri katika suala la usawa katika kutoa nafasi ya kujieleza. "Vyombo vya habari kama hiki, nadhani lengo lake la kwanza ni kuwa huru na kutoegemea upande wowote, kuonyesha usawa, uadilifu na kutoa nafasi ya kujieleza kwa usawa. "

Mbali na radio, CENI tayari inaandaa faili ya kuzindua kituo chake cha televisheni. Faili hiyo tayari iko mikononi mwa Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari.