AFRIKA-ULAYA-ASIA-AMERIKA-VYOMBO VYA HABARI

Wanahabari waendelea kukumbwa na ukatili wa uhalifu

Uturuki sasa ni jela kubwa zaidi duniani kwa waandishi wa habari pamoja na nchi kama vile China, Syria, Misri na Iran, kwa mujibu wa RSF.
Uturuki sasa ni jela kubwa zaidi duniani kwa waandishi wa habari pamoja na nchi kama vile China, Syria, Misri na Iran, kwa mujibu wa RSF. Paul Bradbury/Getty Images

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutokujali kwa Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari, duniani. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa kati ya mwaka 2006-2017 wanahabari zaidi ya 1,000 wameuawa na wengine kutoweka kwa sababu ya kutoa taarifa kwa umma.

Matangazo ya kibiashara

Hali hii imeshuhudiwa pia katika mataifa ya ukanda wa Maziwa Makuu.

Nchini Tanzania, Mwanahahabari wa Gazeti la Mwananchi Azory Gwanda alitoweka mwaka 2017 huku Emmanuel Kibiki wa Gazeti la Raia mwema akiwa hajulikani aliko tangu mwezi Februari mwaka huu.

Nchini Burundi, Mwanahabari wa Gazeti la Iwacu Jean Bigirimana naye hajulikani aliko. Mwezi Agosti, mpiga picha wa Shirika la Reuters James Akena, alipigwa na maafisa wa usalama jijini Kampala nchini Uganda wakati akifanya kazi yake.

Takwimu zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2016 kuhusu usalama wa waandishi wa habari zinaonyesha kwamba kila baada ya siku tano mwandishi mmoja huuawa duniani kote.

Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) linasema Jamal Khashoggi, ambaye aliuawa ndani ya balozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, nchini Uturuki tarehe 2 Oktoba, ni mmoja wa waandishi wa habari 77 na wafanyakazi wa vyombo vya habari ambao wameuawa duniani kote tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

RSF imebaini kwamba asilimia thelathini ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari hauadhibiwi.

UNESCO inasema uhuru wa vyombo vya habari bado umegubikwa na giza na kwamba kasi ndogo ya kushughulikia kesi za mauaji hayo na ongezeko la ukatili wa uhalifu dhidi ya waandishi kunaibua mijadala ya kitaifa pamoja na kulenga kuvinyamazisha vyombo vya habari.

UNESCO inasema usalama wa waandishi wa habari utawezekana ikiwa masuala matatu ya kuzuia, kuwalinda na kuwashitaki wanaohusika yatashughulikiwa.