DRC-UCHAGUZI-CENI-PPRD-SHADARY-KAMPENI

Kamati ya watu 500 yaundwa nchini DRC kumsaidia mgombea wa chama tawala PPRD

Mgombea wa urais kupitia chama tawala nchini DRC PPRD Emmanuel Ramazani Shadary
Mgombea wa urais kupitia chama tawala nchini DRC PPRD Emmanuel Ramazani Shadary Junior D. KANNAH / AFP

Chama tawala nchini DRC cha PPRD, kimetangaza Kamati ya watu 500 watakaomsaidia mgombea wao Emmanuel Ramazani Shadary, kuelekea Uchaguzi Mkuu tarehe 23 mwezi Desemba.

Matangazo ya kibiashara

Kamati hiyo inaundwa na Mawaziri na kuongozwa na Waziri Mkuu Bruno Tshibala, lengo likiwa ni kumsaidia mgombea wao kupata uungwaji mkono na kupigiwa kura wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Miongoni mwa Mawaziri waliopewa jukumu zito katika Kamati hiyo ni Waziri wa Habari Lambert Mende ambaye atakuwa msemaji katika kampeni hiyo.

Kamati hiyo inatarajiwa kuzunguka nchi hiyo nzima, kufanya kampeni ili kuhakikisha kuwa Shadari anamrithi rais Joseph Kabila.

Shadary anayepewa nafasi ya kumrithi rais Kabila, amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na kumzuia kusafiri kwenda katika bara hilo kutokana na tuhma za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo, akiwa Waziri wa Mambo ya ndani.

Hata hivyo, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wa upinzani Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe, ambao haijafahamika iwapo wataungana kuelekea Uchaguzi huo.