BURKINA FASO-USALAMA

Askari wawili wauawa katika mlipuko kaskazini mwa Burkina Faso

Askari wawili wa Burkina Faso wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa huko Nassoumbou, kaskazini mwa nchi hiyo, karibu na mpaka wa Mali, katika mlipuko wa bomu la kienyeji (IED), kwa mujibu wa vyanzo vya usalama.

Vikosi vya usalama na ulini vinaendelea kulengwa katika mashambulizi Ouagadougou, Burkina Faso.
Vikosi vya usalama na ulini vinaendelea kulengwa katika mashambulizi Ouagadougou, Burkina Faso. REUTERS/Joe Penney
Matangazo ya kibiashara

"Gari la jeshi lilikanyaga kifaa cha kulipuka karibu na Nassoumbou", mji wa vijijini ulio kilomita thelathini kutoka Djibo, chanzo cha usalama kimeliambia shirika la Habari la AFP.

"Askari wengine watatu wamejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na wawili ambao wako katika hali mbaya," kimeongeza chanzo hicho, ambacho kimebaini kwamba tukio hilo lilitokea usiku wa kumakia Jumanne wiki hii wakati askari hao walikuwa njiani wakirudi kutoka eneo waliotumwa.

Chanzo cha pili cha usalama kimethibitisha tukio hilo, kikibaini kwamba "vikosi vya ulinzi vimeanzisha operesheni kubwa ya kutegua mabomu katika maeneo ya kaskazini na mashariki".

Burkina Faso, inayopakana na nchi za Mali na Niger, imeendelea kukumbwa na mashambulizi ya hapa na pale ya wanamgambo wa Kiislamu tangu mwaka 2015.

Kulingana na ripoti rasmi iliyotolewa katikati ya mwezi Septemba, mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu yamewaua watu 118, raia 70 na maafisa 48 wa usalama na ulinzi.