DRC-SIASA-USALAMA

DRC yashtumiwa kuwatesa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za biadamu

Mmoja wa waandamanaji aliyejeruhiwa kwa risasi kwenye mguu na polisi wakati wa maandamano ya amani mjini Kinshasa, Februari 25, 2018.
Mmoja wa waandamanaji aliyejeruhiwa kwa risasi kwenye mguu na polisi wakati wa maandamano ya amani mjini Kinshasa, Februari 25, 2018. REUTERS/Goran Tomasevic

Shirika moja la kimataifa linalopinga vitendo vya utesaji na unyanyasaji linaituhumu Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kukumbatia na kutumia njia na mbinu za utesaji dhidi ya wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Shirika hilo la Freedom From Torture, limesema kuwa mamlaka nchini DRC zimekuwa zikitumia mbinu za utesaji ikiwemo ubakaji, vipigo na shoti ya umeme ili kupata taarifa kutoka kwa wanawake na wanaume wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama.

Shirika hilo linazituhumu mamlaka nchini DRC kwa kuwashikilia katika mazingira mabaya wanaharakati wa haki za binadamu huku wengi wakiwa wanazuiliwa bila hata kufunguliwa mashtaka.

Ripoti ya shirika hilo iliyotegemea ushahidi kutoka kwa watu zaidi ya 70 waliokimbia nchi hiyo baada ya kuteswa, wamethibitisha kufanyiwa ukatili ikiwemo kubakwa na kupigwa shoti ya umeme wakati wakihojiwa na vyombo vya usalama.

Ripoti hii inatolewa wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu Desemba 23 mwaka huu, huku tayari kukiwa na tuhuma za watu kutekwa, kubakwa na kuuawa wakiwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama nchini humo.