DRC-ANGOLA-WAKIMBIZI-USALAMA

Hatma ya watoto waliopotezana na wazazi wao mashakani Kasai

Wakimbizi wa DRC nchini Angola wakiwa njiani kuelekea nchini mwao, katika mkoa wa Kasai, baada ya serikali ya Angola kuchukuwa hatua ya kufukuza, Oktoba 31, 2018.
Wakimbizi wa DRC nchini Angola wakiwa njiani kuelekea nchini mwao, katika mkoa wa Kasai, baada ya serikali ya Angola kuchukuwa hatua ya kufukuza, Oktoba 31, 2018. REUTERS/Giulia Paravicini

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yanasema mamia ya watoto ambao walikuwa sehemu ya raia wa nchi hiyo waliofukuzwa kutoka Angola, hawana makazi na wanazurura kwenye mkoa wa Kasai.

Matangazo ya kibiashara

Hali wanayosema imetokana na madhara ya kufukuzwa kwa nguvu na mamlaka nchini Angola, ambazo zinatuhumiwa kuendesha operesheni hiyo bila kuzingatia haki za binadamu.

Taarifa za mashirika hayo zinasema watoto hao ni kati ya umri wa miaka 4 hadi 12 ambao baada ya kufukuzwa Angola, walipotezana na wazazi wao.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Babar Baloch, raia wa DRC walilazimishwa kuvuka mpaka na kurudi kwao baada ya kufukuzwa kutoka Angola.

Uamuzi huo ulitokana na hatua ya Serikali ya Angola ya kuwafukuza wahamiaji wa Kongo, ambao wengi wao walikuwa wakifanya kazi katika sekta isiyo rasmi ya madini katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Angola.

Nchi ya DRC imeapa kuichukulia hatua za kimataifa nchi ya Angola kutokana na kuwafukuza raia wake kwa nguvu huku ikiripotiwa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili.