DRC-SIASA

Uchaguzi DRC: wanasiasa 7 wa upinzani wamtafuta mgombea wao mmoja

Wawili kati ya viongozi wakuu wa upinzani DRC, Vital Kamerhe (kushoto) na Moise Katumbi, Brussels, Septemba 4, 2018.
Wawili kati ya viongozi wakuu wa upinzani DRC, Vital Kamerhe (kushoto) na Moise Katumbi, Brussels, Septemba 4, 2018. JOHN THYS / AFP

Tangu Ijumaa asubuhi, Novemba 9, viongozi wakuu saba wa upinzani wanakutana mjini Geneva, nchini Uswisi, katika moja ya hoteli kubwa katika mji huo. Lengo ni kuafikiana mgombea mmoja atakayepambana na mgombea wa chama tawala, PPRD, katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Desemba 23.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi wa upinzani wamekuwa wakikutana tangu kuwasilisha fomu za uchaguzi Agosti 8, 2018, bila hata hivyo kuafikiana kumteua mgombea mmoja atakayepererusha bendera yao katika uchaguzi wa urais.

Miongoni mwa viongozi hawa saba, baadhi hawamo kwenye orodha ya wagombea watakao wania katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais. Miongoni mwao ni pamoja na Moise Katumbi, gavana wa zamani wa mkoa wa Katanga na Jean-Pierre Bemba, aliyekuwa makamu wa rais, na kiongozi wa zamani kivita. Wengine fomu zao zilikubaliwa na Tume ya Uchaguzi (CENI), ikiwa ni pamoja na Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama cha UDPS.

Viongozi hawa saba, kila mmoja anataka kuwania kwenye nafasi hiyo, hata kama wote wanasema wanamtafuta mgombea mmoja atakaye wania katika uchaguzi wa Desemba 23.

Moise Katumbi anasema kuwa mgombea huyo atateuliwa kati ya viongozi wanne wa upinzani, ambao ni Felix Tshisekedi wa chama cha UDPS Vital Kamerhe wa chama cha UNC, Martin Fayulu kutoka muungano wa upinzani na Freddy Matungulu kutoka Syenco.

Mkutano huo unasimamiwa na Alan Doss, mkuu wa zamani wa MONUSCO, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Kofi Annan Foundation, na tayari alikubali kazi ngumu ya kuwaweka pamoja wanasiasa hawa kwa kumteua mgombea mmoja hadi ifikapo siku ya Jumatatu.