DRC-UCHAGUZI

Kupata mgombea mmoja, viongozi 7 wa upinzani wakutana Geneva

Viongozi wa upinzani wa DRC, Adolf Muzito, Moïse Katumbi, Jean-Pierre Bemba, Vital Kamerhe na Félix Tshisekedi walipokutana Brussels 12 septembre 2018.
Viongozi wa upinzani wa DRC, Adolf Muzito, Moïse Katumbi, Jean-Pierre Bemba, Vital Kamerhe na Félix Tshisekedi walipokutana Brussels 12 septembre 2018. RFI / Léa-Lisa Westerhoff

Viongozi 7 wa upinzani kutoka nchini Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo, wanakutana jijini Geneva, Uswis kwa mazungumzo kuhusu kukubaliana kumteua mgombea mmoja ambaye atapeperusha bendera ya upinzani wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Matangazo ya kibiashara

Wanasiasa hawa wanalenga kuunganisha nguvu ili kutompa urahisi wa kushinda mrithi wa rais Joseph Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary.

Mazungumzo ya awali tayari yamefanyika kwa majuma kadhaa kando na mkutano wa wikend hii, amesema Adolphe Muzito, waziri mkuu wa zamani ambaye amejiunga na upinzani.

Wagombea wanne wa upinzani wamethibitishwa kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa Desemba 23 mwaka huu.

Wagombea hao wa upinzani yumo Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani UDPS, Vital Kamerhe, spika wa zamani wa bunge la kitaifa, mbunge Martin Fayulu na waziri wa zamani wa fedha Freddy Matungulu.

Katumbi, Bemba ambao ni sawa na Muzito, wamezuiliwa na tume ya uchaguzi kugombea kwenye uchaguzi huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo urais na kuwa na kesi za mauaji.

Kwa mujibu wa upinzani kura ya maoni iliyofanyika juma moja lililopita inaonesha kuwa Tshisekedi ataongoza kwa asilimia 36 akifuatiwa na Kamerhe kwa asilimia 17 huku Shadary akifuatia kwa asilimia 16.

Uchaguzi mkuu wa Desemba 23 ni muhimu kwa raia wa DRC ambapo utatoa mustakabali wa baadae wa siasa za nchi hiyo, wakati huu taifa hilo likikabiliwa na changamoto za kiusalama kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kutokana na utajiri wa madini.

Wagombea zaidi ya 20 watachuana kwenye uchaguzi wa mwaka huu ambao utajumuisha pia uchaguzi wa wabunge na ule wa wabunge wa majimbo.

Rais Kabila mwenye umri wa miaka 47 hivi sasa amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, mwaka ambao taiafa hilo lilikuwa linakabiliwa na kashfa za rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Muhula wa pili na wa mwisho wa rais Kabila ulitamatika karibu miaka 2 iliyopita lakini amesalia madarakani kutokana na vipengele vya katiba.

Miezi kadhaa ya kuhusu hatma ya utawala wake ilishuhudia vurugu na maandamano ya kushinikiza aondoke madarakani bila mafanikio, hadi alipotangaza mapema mwaka huu kuwa hatowania tena kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.